Watu watatu wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi na askari wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na kupelekwa hospitali ya Alrahma kwa matibabu.
Majeruhi hao ni Yussuf Ali Juma (23), Ali Shaame Ibrahim (18) na Salim Masoud Bakar (18), wakazi wa Tomondo Wilaya ya Magharibi Unguja.
Kabla ya watu hao kujeruhiwa, milio ya risasi ilitawala majira ya saa 8:30 mchana katika mitaa ya Tomondo, Mwanakwerekwe na Kilimani, hivyo kuzua taharuki miongoni wakazi wa mitaa hiyo.
Mashuhuda wa tukio hilo walidai kuwa waliyaona magari ya vikosi hivyo yakiendeshwa kwa mwendo kasi kuzunguka maeneo hayo huku yakiwa na askari wakifyatua risasi.
“Mimi kwa sasa nipo hapa Kilimani na hivi punde tu risasi tumezisikia kutokea upande huu wa Mwanakwerekwe na Jang’ombe na ghafla naona watu wanakimbizwa kuletwa hapa Alrahma” alisema Rashid Said (54), mkazi wa Migombani ambaye ni dereva teksi.
Majeruhi Ibrahim alisema: “Walikuja wale mazombi, wengine walifunika uso waliwafungua ng’ombe wetu na kutaka kuwachukua, kwanza wakapiga risasi juu, tulipoona wanawapakiza katika magari lao tukasogea ndipo wakatupiga risasi.”
Bakari Juma (35), mkazi wa Msheleshelini alisema: “Tunasikia hawa jamaa wanataka wauze kitoweo cha nyama siku za sikukuu peke yao, lakini miye nasema sawa wafanye hivyo, ila si kwa ng’ombe wa kupora.”
Baadhi ya wananchi walidai kuwa mifugo hiyo wakiwamo ng’ombe wa maziwa ni mali yao.
Mmoja wa wafugaji hao aliyejitambulisha kwa jina moja la Omar alisema: “Sisi tunafuga ng’ombe hawa kama mnavyoyaona mabanda yetu yapo si miaka kumi wala ishirini ni tangu zamani wakati huo Tomondo ni pori tupu na mpaka sasa mifugo yetu haizururi wala haimkeri mtu yeyote.”
Licha ya askari kudaiwa kufika eneo la tukio na katika hospitali walikolazwa majeruhi hao, hali ya usalama ilionekana kuyumba pale makundi ya watu yalipohamasika kusogelea maeneo hayo.
Waliofika katika hospitali hiyo ni pamoja na Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano kwa Umma wa Chama cha Wananchi (CUF), Salim Abdalla Bimani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuahidi kufuatilia zaidi ili kubaini chanzo chake.
Hata hivyo, alisema polisi waliingilia kati na kwenda katika maeneo hayo kurejesha hali ya usalama.
“Sijapata kwa ukamilifu kilichotokea, lakini ni kweli hawa vikosi wanaendesha operesheni ya kukamata ng’ombe wanaozurura mitaani, wamekwenda huko na kukatokea kukwaruzana baada ya kuwepo vijana ambao hawataki kuondoa ng’ombe, nimepeleka askari kutuliza hali na sasa hali imekuwa ya amani”, alisema Kamanda Mkadam.