Thursday, June 09, 2016

SERIKALI NA MIFUKO YA HIFADHI ZA JAMII KUTEKELEZA ADHMA YA KUJENGA UCHUMI WA VIWANDA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Ulemavu), Mhe. Jenister Mhagama akizungumza na Wakurugenzi wa Mifuko ya Hifadhi za Jamii kuhusu adhma ya utekelezaji wa agizo la ujenzi wa uchumi unaotegemea viwanda. Kushoto ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mwigulu Nchemba na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage.
1. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Godius Kahyarara (katikati) akizungumza katika kikao baina ya mifuho ya hifadhi ya jamii na Serikali kilichozungumzia adhma ya utekelezaji wa agizo la ujenzi wa uchumi unaotegemea viwanda. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PPF, Bw. William Urio na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka.
Baadhi ya wajumbe wa kikao cha mashauriano ya pamoja baina ya Serikali na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuhusu adhma ya ujenzi wa viwanda nchini wakifuatilia kwa makini kikao hicho kilichoitishwa na Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Ulemavu). Kikao hicho kilifanyika leo mjini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Godius Kahyarara (katikati) akizungumza katika kikao baina ya mifuho ya hifadhi ya jamii na Serikali kilichozungumzia adhma ya utekelezaji wa agizo la ujenzi wa uchumi unaotegemea viwanda. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa PPF, Bw. William Urio na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya hifadhi ya Jamii (SSRA), Irene Isaka.

Jonas Kamaleki-Maelezo

Serikali imekubaliana na mifuko ya hifadhi ya jamii kuanza utekelezaji wa ujenzi wa viwanda nchini ili kuhakikisha kuwa adhma ya Tanzania ya kufikia uchumi wa viwanda inafanikiwa ifikapo mwaka 2020.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Pombe Magufuli aliyeitaka mifuko hiyo kuwekeza katika ujenzi wa viwanda nchini. 

Akizungumza mara baada ya kikao cha pamoja baina ya Serikali na mifuko hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira, na Ulemavu, Jenister Mhagama alisema Serikali imekusudia kuhakikisha uanzishwaji wa viwanda unaanza haraka na kuongeza fursa za ajira nchini.

Mhagama alisema kuwa mali ghafi na nguvu kazi ya kutosha zipo hapa nchini hivyo hakuna sababu ya kuchelewa kuanza, ambapo Serikali imepanga hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2016, utekelezaji wa adhma hiyo inaanza kuonekana machoni mwa Watanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa sekta ya hifadhi ya Jamii (SSRA)alisema, Irene Isaka alisema ni agizo hilo limekuja katika wakati mwafaka kwa kuzingatia kuwa kwa mifuko ya Hifadhi ya jamii imekusudia kutekeleza kwa vitendo adhma ya Serikali ya awamu ya tano inayosisitiza kuijenga Tanzania kupitia uchumi wa viwanda.

Kwa mujibu wa Isaka alisema kuwa kanuni na mifumo ya mifuko hiyo inaruhusu suala la uwekezaji katika viwanda ama kwa njia ya ubia au ya hati fungani au kutoa mikopo kwa wanotaka kuwekeza katika viwanda.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dkt, Adelhelm Meru alisema uwekezaji katika viwanda ni suala ambalo linawashirikisha wadau wengi zikiwemo wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya malighafi za viwandani, Elimu kwa ajili ya ujuzi wa watu wa kufanya kazi viwandani na Wizara ya Nishati na Madini kwa ajili ya nishati ya kuendesha viwanda.

“Kwa kuangalia raslimali tulizo nazo tumewaomba wadau waanze na viwanda ambavyo vilikuwepo lakini kwa sasa havifanyi kazi kama vile Shirika la Usagishaji la Taifa (NMC), General Tyre, NARCO na Kiwanda cha Viwadudu cha Kibaha, alisema Dr. Meru na kuongeza kuwa malighafi za viwanda hivi zinapatikana hapa nchini.

No comments:

Post a Comment