Monday, June 06, 2016

TANI 70,000 ZA SUKARI ZAAGIZWA ILI KUMALIZA KERO YA UHABA WA SUKARI - WAZIRI MWGULU

Waziri wa Kilimo ,Mifugo na uvuvi Bw Mwigulu Nchemba katikati akizungumza na mpiga kura wake Gaile Elias ambae alipata kumgonga na Baiskeli mwaka 1999 wakati akiwa masomoni na jana wakati wa ziara yake alikutana nae ,kushoto ni katibu wake Bw Daud Ntukuna akishuhudia 

WAZIRI wa Kilimo ,Mifugo na uvuvi Bw Mwigulu Nchemba amewaomba radhi watanzania kwa usumbufu mkubwa walioupata baada ya kuadimika kwa sukari kwa siku miezi michache iliyopita na kuwa serikali inaendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu kwa kuagiza sukari tani 70,000 kutoka nje ya Tanzania.

Mwigulu ambae ni mbunge wa jimbo la Iramba aliyasema haya jana wakati wa ziara yake ya kuwashukuru wananchi wake kwa kumchagua kuendelea kuwa mbunge wa jimbo hilo kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka jana pasipo kufanya kampeni .

Akijibu kero za wananchi wa kijiji hicho cha Kilampanda alisema kuwa kero hiyo ya sukari si kwa kijiji hicho pekee kwani kuna baadhi ya maeneo wananchi walikuwa wakikosa kabisa sukari hata ile inayouzwa kwa bei kubwa japo kwa sasa hali ya upatikanaji wa sukari imeanza kurejea katika hali ya kawaida baada ya serikali kuagiza sukari kutoka nje .

Alisema kuwa kuwa tani zaidi ya 20,000 zimeingia nchini wiki moja iliyopita na hivi sasa tani 15,000 zipo njiani kuingia nchini hivyo bei ya sukari itashuka zaidi ya bei ya sasa baada ya sukari kuingia kwa wingi.

“ Mimi niwahakikishie muda si mrefu hali ya Sukari itarejea katika bei ya kawaida japo wapo baadhi ya watu wananunua akiba ya sukari kwa wingi kwa bei ya sasa ila nawaondoa hofu kuwa sukari itapatikana kwa wingi mbeleni kwani uzalishaji utaanza hivi punde”

Alisema kuwa imekuwa ni kawaida bei kupanda juu zaidi pindi bidhaa zinapoadimika japo ushukaji wake huwa wa kusuasua na katika kukabiliana na uhaba wa sukari na mfumko wa bei serikali imelazimika kuagiza sukari kwa wingi na itaendelea kufanya hivyo ili kuwa na sukari ya ziada ili kutopata adha tena ya sukari.

Hata hivyo alisema kwa kuwa sukari hiyo tano 20,000 zimekwisha ingia na tani 15,000 zipo njiani kuingia suara ya usambazaji linaendelea kufanyika ili kuwafikia wananchi kote nchini ,sukari itakayouzwa kwa bei ilekezi ya serikali.

Awali wananchi wa kijiji hicho cha Kilampanda walimlalamikia waziri huyo kupanda kwa bei ya sukari hadi kufikia kiasi cha Tsh 3000 kwa kilo na kabla ya serikali kutoa bei elekezi sukari kila mfanyabiashara alikuwa akiuza kwa bei yake wengine wakiuza hadi Tsh 4000 kwa kilo jambo ambalo lilikuwa likiwatesa wananchi wenye kipato cha chini.

No comments:

Post a Comment