Tuesday, June 14, 2016

NAIBU SPIKA TULIA ACKSON AKOMAA NA KITI CHA SPIKA KWA SIKU 10


Tangu wabunge wa upinzani waanze kususa vikao vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, kiongozi huyo wa Bunge ameamua ‘kukomaa’ na kiti hicho, hatua inayosababisha wapinzani wasipate fursa ya kutia mguu bungeni.

Kwa kawaida, Spika wa Bunge, Job Ndugai au naibu wake wanapokuwa na shughuli nyingine, huachia kiti hicho kwa wenyeviti watatu wa Bunge kuendesha vikao, lakini safari hii Dk Tulia amekuwa akiingia kila siku asubuhi na jioni.

Mei 31, mwaka huu wabunge wote wa upinzani walianza kususa vikao vinavyoendeshwa na kiongozi huyo kwa madai ya kutokuwa na imani naye, hasa baada ya kuzuia hoja ya kufukuzwa kwa wanafunzi 7,802 katika chuo cha Udom.

Hoja hiyo iliwasilishwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari lakini Dk Tulia alisema haikuwa na umuhimu kwa wakati huo, jambo lililozua tafrani baina ya kiongozi huyo na wabunge wote wa upinzani.

Kutokana na hali hiyo, wabunge hao walipitisha azimio la kususa vikao vinavyoendeshwa na kiongozi huyo na tangu siku hiyo, kila anapoingia bungeni kuongoza kikao wamekuwa wakitoka ukumbini.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye kwa sasa yuko nchini India kwa matibabu, amekuwa akisaidiwa na Dk Tulia pamoja na wenyeviti watatu wa Bunge ambao ni Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu, Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge na  Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Najma Giga. 

Tangu wapinzani waamue kususa vikao vinavyoendeshwa na Dk Tulia, kiongozi huyo wa Bunge amekuwa akiendelea kuongoza vikao na kuwafanya wapinzani kila siku kutoka katika ukumbi huo.

Hata hivyo Dk Tulia alieleza bungeni kuwa kama kuna mbunge yeyote ambaye anahisi hatendewi haki, kanuni za Bunge zinatoa nafasi namna ya kuwasilisha malalamiko yake.

Kutokana na hali hiyo, wabunge wa upinzani kupitia kwa Mbunge wa Simanjiro (Chadema), James Millya waliwasilisha hoja kwa Spika ya kuazimia kumng’oa madarakani Naibu Spika.

Hoja sita za Millya zilipokelewa na ofisi ya Katibu wa Bunge kwa niaba ya Spika ambaye yuko nje, zikibainisha kuwa wabunge hao hawana tatizo na kiti bali Dk Tulia.

Spika Ndugai atatakiwa kuwasilisha barua hiyo ya kusudio la kumng’oa Dk Tulia katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa ajili ya kushughulikiwa.

Pamoja na suala lake kupelekwa kwenye kamati hiyo, Dk Tulia alitoa mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Nkasi Kaskazini(CCM), Ally Keissy kuhusu posho kwa wabunge wote wa upinzani wanaoingia na kutoka nje bila kufanya kazi. Alisema wabunge ambao hawashiriki vikao vya Bunge hawatalipwa posho.

No comments:

Post a Comment