Thursday, June 09, 2016

WAZIRI LUKUVI AZINDUA BARAZA LA ARDHI WILAYA YA KITETO MKOANI MANYARA

 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi akisalimiana na Mpima ardhi mkuu wa kanda ya kaskazini Nina Rutakyamirwa, alipofika wilayani Kiteto kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya hiyo (kushoto) ni mkuu wa Mkoa huo, Dk Joel Bendera.
 Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi akisalimiana na Kaimu Msajili msaidizi wa baraza la ardhi na nyumba wa kanda ya kaskazini Zena Happe alipofika wilayani Kiteto kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya hiyo (kushoto) ni mkuu wa Mkoa huo, Dk Joel Bendera.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi akimtambulisha kwa wananchi Mwenyekiti wa Baraza la ardhi na nyumba la Wilaya ya Kiteto Charles Mnzava, alipozindua baraza hilo.

WANANCHI wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara waliokuwa wanasafiri kwa kilometa 320 kwenda Wilayani Simanjiro na kurudi kufuata huduma ya Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya, hvi sasa wamemaliziwa kero hiyo baada ya Wziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi, William Lukuvi kuzindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kiteto.

Waziri Lukuvi akizungumza wakati akizindua baraza hilo alisema, kero ya wananchi wa wilaya ya Kiteto kufuata huduma hiyo umbali wa kilometa 320 kwenda na kurudi wilayani Simanjiro ambapo kuna baraza kama hilo, ili kufungua mashauri yao kwenye masuala ya ardhi au nyumba limemalizika.

“Baraza hilo litawasaidia wananchi wa Kiteto kuondoa kero ya kufuata huduma hiyo wilayani Simanjiro kwani kati ya kesi 150 zinazofanyika kwa mwaka wilayani Simanjiro, kesi 100 zinawahusu watu wa wilaya ya Kiteto,” alisema Lukuvi.

Alisema mpango wa matumizi bora ya ardhi utasababisha wakulima na wafugaji kutogombana kwani kila kijiji kitatenga eneo la mashamba, malisho ya mifugo, makazi, sehemu za ibada na huduma nyingine na kuondokana na migogoro.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera alisema baraza hilo litasaidia kumaliza tatizo la migogoro ya ardhi iliyokithiri kwani awali wananchi wengi walikuwa wanafika mjini Babati kutoa malalamiko yao ya migogoro ya ardhi.

Dk Bendera aliwataka Mwenyekiti wa baraza hilo la Kiteto Charles Mnzava na wazee wa baraza kutenda haki kwa wananchi wa Kiteto wakati wa kuendesha mashauri hayo ili jamii ione faida ya kuwepo kwa baraza hilo.

Hata hivyo, Mbunge wa jimbo la Kiteto, Emmanuel Papian alimshukuru Waziri Lukuvi kwa kuzindua baraza hilo kwani litasaidia kwa namna moja au nyingine kumaliza migogoro ya ardhi ambayo ilikuwa imekithiri kwenye eneo hilo la Kiteto.

Papian alisema kupitia baraza la ardhi na nyumba hapa Kiteto huo ndiyo utakuwa mwisho wa kuwepo kwa migogoro ya ardhi kwani awali walikuwa wanateseka kwenda Simanjiro kwani jamii ilikuwa inatumia gharama kubwa.

No comments:

Post a Comment