Wednesday, June 08, 2016

BUNGE LAKANUSHA UVUMI ULIOENEA KUHUSU AFYA YA SPIKA WA BUNGE JOB NDUGAI:

Ofisi ya Bunge imesema Spika wa Bunge, Job Ndugai anatarajiwa kurejea nchini muda wowote akitokea India alipokuwa akifanya uchunguzi wa afya yake.

Taarifa hiyo ya Bunge imekuja siku moja baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikieleza kuwa kiongozi huyo yuko katika hali mbaya, jambo ambalo limeelezwa siyo kweli. Takribani wiki ya tatu sasa, Ndugai hajaonekana bungeni.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Bunge, Owen Mwandumbya alisema jana kuwa kiongozi huyo amekwenda India kwa uchunguzi.

Alisema Spika aliporejea kutoka India Desemba mwaka jana, alitakiwa kurudi tena baada ya muda kwa ajili ya uchunguzi.

“Atarudi muda wowote kuanzia hivi sasa kwani yuko nchini India,” alisema Mwandumbya.

Alifafanua kuwa hali ya spika iko vizuri na hivi sasa anafanya mambo ya kawaida ili aweze kurejea nchini.

Mwaka jana baada ya Ndugai kuwasili kutoa India, alisema afya yake iko imara na anaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu na madaktari.

No comments:

Post a Comment