Saturday, June 25, 2016

WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO YATOA ELIMU YA UBIA KATI YA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI KWA WABUNGE


Mgeni Rasmi, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson akifungua Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kuhusu Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma ilifofanyika leo Mjini Dodoma katika ukumbi wa Pius Mswekwa ikiwa na Lengo la kuwajengea uwezo wabunge kuhusu umuhimu wa kushirikisha Sekta Binafsi katika miradi ya maendeleo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Uratibu Bunge Vijana Kazi Ajira na Walemavu Mhe. Jenista Mhagama(wa kwanza kushoto) akifuatilia Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango ikilenga kuwajengea uwezo wabunge kuhusu umuhimu wa kushirikiana kati ya Sekta Binafsi na ile ya Umma (PPP) Katika miradi ya maendeleo. Kulia ni Spika wa Bunge Mhe. Tulia Ackson ambaye alikuwa mgeni rasmi katika semina hiyo. 
Mbunge wa Ileje Mhe. Janet Mbene akitoa maoni yake wakati wa semina ya kuwajengea uwezo wabunge kuhusu umuhimu wa kushirikisha Sekta Binafsi katika miradi ya maendeleo. 
Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Sophia Simba akitoa maelezo jinsi miradi itakayotekelezwa kwa ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi inavyoweza kuchangia kukuza maendeleo. 
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tulia Ackson (katikati) ambaye alikuwa mgeni rasmi wa semina ya kuwajengea uwezo Wabunge kuhusu umuhimu wa Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma (PPP) akifurahia jambo mapema  Bungeni Mjini Dodoma. Kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Servacius Likwelile na kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bajeti Mhe. Josephat Kandege. 
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti Mhe. Josephat Kandege akiwakaribisha wajumbe kutoa maoni katika Semina iliyoandaliwa na Wizara ya Fedha na Mipango kwa lengo la kuwajengea uwezo Wabunge kuhusu umuhimu wa ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma. Kulia ni Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson ambaye alikuwa Mgeni Rasmi kwenye semina hiyo.( Picha na Frank Mvungi-Dodoma )


Wizara ya Fedha na Mipango leo Mjini Dodoma imetoa semina Kuhusu ubia kati ya Sekta Umma na Sekta Binafsi kwa wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Semina hiyo iliyofunguliwa na Naibu Spika Mhe. Tulia Ackson ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye semina hiyo ambapo mada kuhusu utaratibu huo iliwasilishwa na Kamishna anasimaia Idara inayoratibu ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi kutoka Wizara hiyo Dkt. Frank Mhilu.

“Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi ni mkataba wa muda mrefu wa kuanzia miaka 5 hadi 30 na kuendelea kati ya kampuni ya mwekezaji binafsi na Taasisi ya Serikali ambapo mwekezaji binafsi anajenga miundombinu au anapewa miundombinu ili aiboreshe kwa lengo la kutoa huduma ya umma kwa gharama nafuu na baada ya mkataba kwisha miundombinu husika hurejeshwa kwa Serikali,” alifafanua Dkt. Mhilu.

Aidha Dkt. Mhilu aliendelea kusema kuwa, ili kufanikiwa katika ubia lazima kuwe na maandalizi muhimu ambayo ni kuibua fursa za uwekezaji kwa mujibu wa mpango wa Taifa wa maendeleo, kufanya uchambuzi yakinifu ili kujiridhisha kuwa mradi una manufaa kwa uwekezaji kwa utaratibu wa ubia.Vile vile kuandaa ardhi na miundombinu wezeshi, kutangaza miradi kwa uwazi, kujiridhisha ubora wa zabuni ya mwekezaji na namna ambavyo fedha zitapatikana na uwezo wa Taasisi ya Umma kusimamia mradi husika.

Pia Dkt. Mhilu aliitaja miradi ambayo iko katika hatua mbalimbali za ubia kuwa ni mradi wa mabasi ya haraka Dar es Salaam (DART), mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi III (TANESCO), mradi wa barabara ya tozo wa Dar – chalinze (TANROADS), mradi wa uzalishaji wa madawa muhimu (MSD) pia iko miradi ambayo imechambuliwa na kutolewa taarifa zake kwa ajili ya kuboreshwa.

Dkt. Mhilu amesema kuwa utaratibu wa ubia sasa utakuwa kwenye ofisi moja ambayo ni Wizara ya Fedha na Mipango ili kuweka ufanisi katika utekelezaji wake ikiwa ni maamuzi ambayo yamefanyika katika awamu ya Tano ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Miradi ya ubia ni mkombozi katika kuboresha Bajeti ya Serikali na kuharakisha maendeleo endapo tu fursa za uwekezaji zitabuniwa vizuri, miradi itaandaliwa vizuri na taarifa sahihi zitatumika katika kuandaa miradi, wawekezaji wapatikane kwa njia ya haki, uwazi na ushindani pamoja na mwekezaji kusimamiwa vyema katika ujenzi, uendeshaji na urejeshaji wa miundombinu.

No comments:

Post a Comment