Saturday, June 04, 2016

PROF.MBARAWA:BARABARA YA IRINGA- DODOMA KILOMITA 260 KUFUFUA UCHUMI WA MIKOA HIYO

Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mkoani Iringa. Kulia ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi na Kushoto Mkuu wa mkoa wa Iringa Bi Amina Masenza.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.William Lukuvi akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa mara baada ya kuanza ziara ya siku nne mkoani Iringa.

Waziri Wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akimsikiliza Meneja wa wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole wakati wa ukaguzi wa barabara ya Dodoma –Iringa KM 260 ambapo ujenzi wake umekamilika kwa kiwango cha lami.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza akitoa taarifa ya hali ya Miundombinu kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati wa ziara ya waziri huyo katika mkoani Iringa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wakazi wa mikoa ya Dodoma na Iringa kutumia fursa ya kukamilika kwa kiwango cha lami barabara ya Dodoma Iringa kufanya shughuli za uzalishaji ili kujiletea maendeleo.

Akizungumza wakati akikagua barabara ya Dodoma Iringa KM 260 Profesa Mbarawa amesema Barabara hiyo imelenga kufufua uchumi wa mikoa ya Iringa na Dodoma hususani hifadhi ya Ruaha na Vivutio vya utalii vilivyopo mkoani Iringa.

“Barabara hii tuIiigawa katika sehemu tatu Iringa-Migori KM 95.2, Migori- Fufu KM 93.8 na Fufu –Dodoma Km 70,9 ili ikamilike kwa haraka na hivyo kuharakisha maendeleo ya watu wa Dodoma na Iringa “. Amesema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amesema kiasi cha sh. bil 4.6 itatolewa na Serikali ili kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha ujenzi wa barabara ya Iringa mchepuo KM 7.3 itakayoanzia Kihesa –Kilolo kupitia Chuo Kikuu cha Iringa hadi Igumbilo ili kuondoa msongamano wa magari katikati ya Mji wa Iringa.

Waziri Mbarawa amesisitiza nia ya Serikali ya kuukarabati uwanja wa Ndege wa Nduli mkoani Iringa ili kuwawezesha watalii wanaokwenda katika hifadhi ya Ruaha na Vivutio vingine vya Utalii Mkoani Iringa kutumia uwanja huo ili kuhamasisha uchumi wa mkoa wa Iringa.

Naye Mbunge wa Isimani Mhe. Wiliam Lukuvi ambaye ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Iringa amemshukuru Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Mbarawa kwa kukubali kujenga barabara ya Mchepuo ya Iringa na kumuomba aangalie uwezekano wa kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Iringa-Kalenga hadi katika hifadhi ya Taifa Ruaha yenye urefu wa KM 104.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Bi. Amina Masenza amemuomba Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupanua barabara ya TANZAM eneo la Mlima kitonga na kumalizia ujenzi wa barabara ya Tosamaganga –Ugwachanya kwa kiwango cha lami na Ujenzi wa daraja la Tosamaganga ili kupunguza changamoto za usafiri kwa wakazi wa Iringa.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano yupo katika Ziara ya siku nne mkoani Iringa kukagua maendeleo ya Ujenzi wa Miundombinu mkoani humo.

No comments:

Post a Comment