Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza katika Mkutano wa Mwaka wa Wachumi na Maafisa Mipango unaofanyika katika ukumbi wa Hazina mjini Dodoma. Alifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mge. Dkt. Philip Mpango. Kaulimbiu ya Mkutano ni Kuelekea kwenye Utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servacius Likwelile akimkaribisha Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Harrison Mwakyembe kufungua mkutano huo. Kulia kwake ni Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri akizungumza katika mkutano wa Mwaka wa Wachumi na Maafisa Mipango unaofanyika mjini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa mkutano wa Mwaka wa Wachumi na Maafisa Mipango wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe.
Na Benny Mwaipaja, WFM.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Servacius Likwelile amesema kuwa Tanzania imejipanga kuimarisha mapato yake ya ndani ili kutekeleza kikamilifu Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021.
Dkt. Likwelile, amesema hayo Mjini Dodoma, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku 2 unaowahusisha wataalamu wa Uchumi na Mipango wapatao 170 kutoka nchi nzima.
Amesema kuwa misaada kutoka kwa wadau wa maendeleo imekuwa ikipungua kila wakati, hatua ambayo imeifanya Serikali kuendelea kujipanga kukabiliana na nakisi ya Bajeti yake ili kukuza maendeleo.
"Mikopo yenye riba nafuu nayo imepungua, sasa hivi unaenda kukopa kibiashara, kwa uchumi wetu huu hatuwezi kumudu" alisisitiza Dkt. Likwelile.
Ameeleza kuwa Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuimarisha miundombinu ya barabara, reli, bandari na mambo mengine, hali inayohitaji fedha nyingi ambazo zitapatika kwa kukusanya kodi mbalimbali.
Amewataka wataalamu hao wa uchumi na mipango kujadili na kuibuka na mipango itakayosaidia kufanikisha utekelezaji wa Mpango huo wa Pili wa Maendeleo wa Taifa unaotarajiwa kugharimu shilingi Trilioni 107.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amewataka wataalamu hao kutoa mapendekezo ya kitaalamu wakizingatia changamoto mbalimbali zikiwemo za kupanda kwa gharama za mafuta duniani.
Vilevile, amewakumbusha umuhimu wa kutumia takwimu sahihi wakati wa kupanga namna bora ya kutekeleza mpango huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa na watanazania kuwaletea maendeleo ya haraka.
"Takwimu ndizo zinazotoa picha halisi ya matatizo yanayowakabili watanzania ukiwemo umasikini, ambapo zikitumika vizuri zitasaidia kupanga namna bora ya wananchi wanavyoweza kuondokana na umasikini huo" Alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri, amesema kuwa Tanzania imedhamiria kuwa nchi yenye uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.Amesema kuwa hatua hiyo itafikiwa kwa kuelekeza nguvu kubwa katika uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Mwanri amesema kuwa hatua hiyo itakuza uchumi wa nchi kwa kuongeza kipato cha wananchi pamoja na ajira na akasisitiza umuhimu wa wananchi kufanya kazi kwa bidii na kujitolea utaalamu na nguvu zao zote kufanikisha malengo hayo.
No comments:
Post a Comment