Serikali imeunda kikosi kazi kwa ajili ya kushughulikia uharibifu wa kimazingira ikiwemo kudhibiti uvuvi haramu wa kutumia mabomu ili kulinda mazalia ya samaki na kulinda ikolojia ya bahari.
Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mhe. Wiliam Ole Nasha alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Chambani (CCM), Mhe. Yusuf Salim Hussein aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kuzuia uvuvi haramu wa kutumia mabomu.
Ole Nasha alitaja wajumbe wanoaunda kikosi kazi hicho kuwa ni Ofisi ya Rais, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Wizara za Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Wizara ya Nishati na Madini.
Alizitaja Ofisi nyingine kuwa ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), ambapo kikazi kazi hicho kitaratibiwa na Ofisi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini.
“Kuna uhusiano mkubwa kati ya ugaidi na uvuvi wa kutumia vilipuzi, hivyo suala hili ni la kiusalama zaidi na kwa kutambua hilo Serikali imeanzisha vituo 5 vya kudhibiti uvuvi huo na baadhi ya vituo hivyo viko Pemba na Tanga,” alisema Ole Nasha.
Ole Nasha alisema inaendelea kuziagiza Halmashauri za Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi kushirikiana na jamii kusimamia kwa ukamilifu udhibiti wa uvuvi haramu wa kutumia mabomu kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wanaojihusisha na uvuvi huo.
“Sheria ya Uvuvi ya Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za Mwaka 2009 zimekasimu Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Raslimali za Uvuvi katika Halmashauri zote nchini,”Alisema Ole Nasha.Alisema kuwa Wizara ina jukumu la kuanda Sera, Sheria, Kanuni zinazotumika katika Uhifadhi, Udhibiti na Usimamizi wa waza Uvuvi nchini.
Ole Nasha aliongeza kuwa ili kuongeza nguvu ya kudhibiti uvuvi haramu, Serikali ilianzisha mfumo wa kushirikisha jamii kupitia vikundi vya usimamizi shirikishi wa Raslimali za Uvuvi (BMUs) ili kuwaelimisha wananchi juu ya athari ya matumizi ya mabomu na uvuvi haramu.
Alisema matumizi ya mabomu katika uvuvi yana athari kubwa kwa samaki na mazingira ya baharini kwa kuwa huua samaki na viumbe wengine na uharibu matumbawe ambayo ni mazalia ya samaki.
Ole Nasha alibainisha athari nyingine kuwa ni kupungua kwa rasilimali za uvuvi, kupoteza kipato, kuongezeka kwa mmomonyoko wa fukwe za bahari, pammoja na kuathiri afya za walaji.
No comments:
Post a Comment