Elimu, Utafiti Na Uongozi,
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ndugu waandishi wa
habari, nimewaita hapa kuelezea masikitiko makubwa kutokana na kauli za hivi
karibuni za aliyekuwa waziri wa mambo ya nje ndugu Bernard Membe. Akifanya
mahojiano na kunukuliwa na gazeti la Mwananchi la tarehe 22 na 23 Januari, 2016
, ndugu Membe amekaririwa akitoa kauli zenye maudhui ya kubeza juhudi za mh.
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli na kufutwa kwa
uchaguzi wa Zanzibar. Kauli hizi zilijikita katika maeneo makubwa manne kama
ifuatavyo:-
1. Ndugu Membe
amebeza juhudi za Rais Dr. John Magufuli za kupunguza ukubwa wa serikali,
na kwamba hatua yake ya kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri haijasaidia
chochote kwa taifa. Na kwamba ni sawa na kupunguza idadi ya mifuko huku idadi
ya mayai ikiwa ni ile ile.
2. Ndugu Membe
amekosoa na kubeza hatua ya serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dr.
Magufuli ya kupunguza safari za nje zisizo za lazima na tija kwa taifa, na
kwamba safari hizo zilikua na neema kubwa kwa watanzania.
3. Ndugu Membe
amepinga kufutwa kwa matokeo yote ya uchaguzi visiwani Zanzibar na kudai kwamba
dunia nzima inatushangaa kwa uamuzi huo.
4. Ndugu Membe
amekosoa mazungumzo ya kutafuta maridhiano baina ya Chama cha CUF na CCM
visiwani Zanzibar huku akidai kuwa ni makosa kuwaachia Rais wa Zanzibar Dr. Ali
Mohammed Shein na Maalim Seif Shariff Hamad kufanya mazungumzo peke yao.
Tumesikitishwa sana na
kauli hizo na vijana wasomi tumeamua kumjibu kama ifuatavyo:-
KUPUNGUZA UKUBWA WA
SERIKALI
Rais Dr. John Magufuli
amechukua juhudi za kupunguza ukubwa wa serikali kwa kuanza na baraza la
mawaziri. Idadi ya mawaziri imepungua kutoka mawaziri 60 wakati wa serikali ya
awamu ya nne hadi mawaziri 34 tu katika serikali ya awamu ya tano. Punguzo hili
ni idadi ya mawaziri 26.
Gharama za kawaida za
kumuhudumia waziri zilizopungua:
a. Kila waziri na naibu wake hupewa gari
aina ya GX V8 ambalo thamani yake inakadiriwa milioni 400. Gari hili linahitaji
mafuta na gharama ya kulitunza. Hivyo magari 26 yamepungua ambayo gharama
yake ya manunuzi na matunzo ni mabilioni ya pesa.
b. Nyumba ya kuishi. Mawaziri wote wanapewa
nyumba na serikali. Nyumba hizo zinalipiwa umeme na maji
c. Wasaidizi wa mawaziri. Kila waziri
anapewa katibu wake, hivyo serikali imepunguza nafasi 26 za makatibu kwa
kupunguza mawaziri 26. Hawa wanalipwa mishahara na posho.
d. Madereva. Kila waziri ana dereva wa
serikali anayelipwa mshahara na posho awapo nje ya kituo cha kazi. Hivyo
serikali imepunguza mishahara na posho za watu 26.
e. Kila waziri anapewa ulinzi nyumbani kwake
wa askari wawili wa jeshi la polisi masaa 24. Hivyo kwa kupunguza mawaziri 26,
tumepunguza askari 52 ambao sasa watakwenda kuongeza ulinzi wa raia na mali za
wananchi wengine.
f. Kila waziri anatengewa mafungu ya fedha
kwa ajili ya mawasiliano, safari zake za kikazi, ziara za mikoani, vikao na
majukumu mengine ya kazi ambayo ni mamilioni ya shilingi kila mwezi. Kwa
kupunguza mawaziri 26 Rais ameokoa mamilioni ya shilingi kila mwezi.
g. Gharama za kuwahudumia mawaziri 26 wakiwa
bungeni Dodoma pia zimepungua.
WIZARA
ZILIZOUNGANISHWA
Katika muundo wa baraza
la mawaziri la Dr. John Pombe Magufuli alilolitangaza , ziko wizara 5
ambazozimeunganishwa pamoja. Wizara hizi ni
a. Kilimo, Mifugo
na Uvuvi (wizara 3 zimeunganishwa, sasa zina waziri 1)-Mh. Mwigulu Nchemba
b. Wizara ya mambo
ya nje, kikanda na kimataifa (wizara mbili zimeunganishwa, sasa zina waziri 1)-
Mh. Augustine Mahiga
c. Wizara ya
viwanda, biashara na uwekezaji (wizara 2 zimeunganishwa,sasa zina waziri 1)-
Mh. Charles Mwijage
d. Wizara ya elimu,
sayansi, teknolojia na ufundi (wizara 2 zimeunganishwa, sasa zina waziri 1)-
Mh. Joyce Ndalichako
e. Wizara ya
ujenzi, mawasiliano na Uchukuzi (wizara 3 zimeunganishwa, sasa zina waziri 1)
-Mh. Makame Mbarawa
Katika hali hiyo, ni
dhahiri idadi ya mawaziri imepungua na hivyo gharama ya kuwahudumia pia
imepungua. Kutoka hadharani na kusema hakuna kilichopungua ni upotoshaji mkubwa
ambao mtu mwenye uelewa wa kawaida kabisa anaweza kuubaini.
IDADI YA MAKATIBU WAKUU
Makatibu wakuu na
manaibu waliohudumu wizara wakati wa serikaliya awamu ya nne walikua jumla ni
54. Mh. Rais Dr. Magufuli ameteua makatibu wakuu 29 na manaibu 21. Hivyo hapa
pia idadi imepungua na kufanya gharama kupungua pia.
WATANZANIA WANAMSHANGAA
MEMBE
Kitendo cha ndugu
Bernard Membe kudai kuwa kupungua huku kwa ukubwa wa baraza la mawaziri
hakujasaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa serikali, ni jambo la ajabu
ambalo watanzania wote wanalishangaa na kuliona kuwa ni uongo na upotoshaji
mkubwa. Upotoshaji huu unastahili kupuuzwa na kila mpenda mabadiliko ya kweli.
Baada ya Mh. Raisi
kuteua baraza lake la mawaziri mwezi desemba, mwanazuoni profesa Samuel
Wangwe alikaririwa na gazetila Habari Leo la tarehe 11 Desemba, 2016
akisifu Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli kupunguza
idadi ya mawaziri.
Profesa Wangwe alisema
mawaziri ni watu wa kusimamia sera, na watendaji wakubwa ni makatibu wakuu.
Aidha, wanaharakati na wadau mbalimbali wote walipongeza kupunguzwa huko kwa
baraza la mawaziri wakisema taifa limepunguza mzigo. Lakini ajabu, ndugu
Bernard Membe hajaliona hilo. Inasikitisha sana.
Wakati mwingine inatufanya
tujiulize, ndugu Membe ambaye alikua miongoni mwa wana CCM waliowania kuteuliwa
na Chama kugombea Urais wa Tanzania, na baadae kushindwa kwa kura ndani ya
Halmashauri Kuu ya CCM taifa, amesema maneno haya kwa malengo au makusudio
yapi? Waswahili wanasema, aliyepata kapata. Tunamtaka ndugu Membe ajiunge na
watanzania kukubali kuwa Dr. Magufuli ndiye Rais wa nchi yetu aliyechaguliwa na
wananchi. Hivyo amuache atimize wajibu wake kwa taifa.
KUPUNGUZA SAFARI ZA NJE
Katika hatua nyingine ya
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini, Raisi ameagiza kufutwa kwa
safari zote zisizo za tija kwa nchi, na kwamba safari zote zitatolewa kwa
kibali maalum cha Raisi.
Kwa mujibu wa hotuba ya
Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli bungeni mjini Dodoma,
safari za nje za miaka miwili pekee (2013-2015) ndugu Membe akiwa waziri wa
mambo ya nje, shilingi bilioni 356.324 zilitumika kwa safari za nje huku tiketi
za ndege peke yake zikigharimu bilioni 183.160.
Taasisi zilizoongoza kwa
matumizi hayo ni pamoja na wizara ya mambo ya nje aliyokuwa anaihudumia ndugu
Membe. Tunajiuliza, ni trilioni ngapi zilitumika kwa safari za nje katika
kipindi chote cha miaka 8 ambacho ndugu Membe alikuwa waziri? Je, huu haukua mzigo
kwa taifa? Ndugu Membe anazungumziaje matumizi haya mabovu ambayo yalifanyika
yeye akiwa na dhamana ya wizara hiyo?
Watanzania wote
tunafahamu na kukubali kuwa safari hizi zilikua mzigo mkubwa kwa taifa, na
tunaunga mkono juhudi za kupunguza na kudhibiti safari zisizo za lazima.
BERNARD MEMBE
SI MKWELI
Ndugu waandishi, ili
kudhihirisha kuwa ndugu Bernard Membe si mkweli kwa anayoyasema kuhusu safari
za nje, na kwamba kauli zake kuhusu jambo hili zinakinzana, baada ya hotuba ya
Rais Dr. John Magufuli bungeni mjini Dodoma, bwana Membe alinukuliwa
akimpongeza mh Rais kwa uamuzi wake wa kupunguza safari za nje kwani kwa maneno
yake alisema walikua wanapishana angani kama vile nyumbani kunawaka moto.
Ni Bernard Membe
huyuhuyu ambaye leo anatafuna maneno yake bila aibu na kutueleza kuwa safari
zile zilikua na neema kwa taifa.
KUHUSU KUTOKUA NA BALOZI
KATIKA NCHI ZOTE
Katika kuhalalisha
safari za nje zisizo za lazima, ndugu Membe alieleza kuwa Tanzania ina mabalozi
36 tu katika nchi 194 ambazo tunapaswa kuwa na mabalozi.
Tunapenda kumfahamisha
ndugu Membe kuwa kutokuwa na balozi katika nchi zote sio kigezo cha kutumia
mabilioni ya pesa kwa ajili ya safari zisizo na tija kwa taifa. Kutokana na
kuwa uchumi wetu bado unakua, na haustahamili gharama za kuweka mabalozi katika
nchi zote, wako mabalozi wetu nje ya nchi ambao wanawakilisha nchi zaidi ya
moja zilizoko katika ukanda mmoja. Mfano, balozi Ombeni Sefue aliwahi kuwa
balozi wetu Marekani akiwakilisha pia CUBA. Aidha, uamuzi wa nchi kufungua
ubalozi katika nchi nyingine hutegemea vigezo mbalimbali kama faida za
kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kidiplomasia.
RAISI HAJAKATAA KUSAFIRI
NJE YA NCHI
Ndugu Membe anapotosha
ukweli anaposema Tanzania sio kisiwa na kwamba Raisi na waziri wake wa mambo ya
nje lazima wasafiri nje ya nchi watake wasitake.
Tunapenda kumfahamisha
ndugu Membe kuwa, mh. Raisi Dr. John Magufuli hajatoa kauli kuwa yeye au
wasaidizi wake hawatosafiri nje ya nchi katika safari za muhimu na zenye tija.
Isipokuwa, muongozo wa mh. Rais kuhusu safari za nje unalenga kupunguza safari
zile ambazo hazina ulazima na tija kwa taifa.
KUHUSU MGOGORO WA
UCHAGUZI WA ZANZIBAR
Katika maelezo
aliyonukuliwa na gazeti la Mwananchi, ndugu Membe alieleza kupinga kufutwa kwa
matokeo yote ya uchaguzi wa Zanzibar yakiwemo ya wawakilishi, na kwamba jambo
hili limeihuzunisha dunia.
Kauli hii ya ndugu Membe
inatushangaza na kutusikitisha sana. Kwanza tunajiuliza, Je, ikiwa sehemu kubwa
ya uchaguzi iligubikwa na udanganyifu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi
kinyume na sheria za uchaguzi wa Zanzibar, ni kwanini ndugu Membe ashangae
uchaguzi wote kufutwa na tume ya uchaguzi ZEC?
Tunamtaka ndugu Membe
atueleze, ni dunia ipi hiyo inayotushangaa?
Ni kwanini dunia hiyo
anayoitetea ndugu Membe haijashangaa kumuona maalim Seif Shariff Hamad
akijitangaza kuwa mshindi kinyume cha sheria za uchaguzi?
Ndugu Membe anapaswa
kushangaa, ni kwanini hadi leo hii maalim Seif Shariff Hamad hajakamatwa
na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya kujitangaza kuwa mshindi kinyume
cha sheria.
KUHUSU VIKAO VYA
MARIDHIANO
Kuhusu vikao vya
maridhiano vilivyokua vinaendelea, ndugu Membe amekosoa kitendo cha Raisi wa
Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar na maalim Seif Shariff hamad kuachwa
wakazungumza wenyewe wawili.
Kwanza tunasikitika kuwa
ndugu Membe huenda ama hajui kinachoendelea Zanzibar au ameamua kupotosha umma kwa
makusudi. Hii ni kwasababu mazungumzo yaliyokua yakiendelea Zanzibar,
hayakuwahusisha Dr. Shein na maalim Seif Shariff peke yao. Bali yalishirikisha
marais wastaafu wa Zanzibar, Raisi wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Makamu
wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar.
Pili, katika muafaka wa
kisiasa wa Zanzibar wa mwaka 2009/2010 uliopelekea kuundwa kwa serikali ya
umoja wa kitaifa, kwa kiasi kikubwa ni maalim Seif Shariff hamad na Rais wa
Zanzibar wa wakati huo mh. Amani Abeid Karume pekee walioshiriki mazungumzo.
RAI KWA NDUGU MEMBE
Mosi, tunapenda
kumkumbusha ndugu Bernard Membe kuwa yeye ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM
taifa amewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ya CCM. Hivyo anajua utaratibu wa Chama
na anayo nafasi ya kuyasema mawazo yake juu ya uendeshaji wa serikali ndani ya
vikao halali vya chama. Aidha, ndugu Membe kwa nafasi yake kama mjumbe wa NEC
na waziri wa zamani wa mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa, anayo
nafasi ya kutoa ushauri na maoni yake moja kwa moja kwa Raisi wa jamhuri ya
muungano wa Tanzania mh. Dr. John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM taifa Dr. Jakaya
Kikwete au kwa Katibu Mkuu wa CCM ndugu Abdulrahman Kinana.
Kutotumia fursa hizo
kutoa maoni yake ni kujishushia heshima mbele ya jamii.
Pili, tunamkumbusha
ndugu Membe kuwa yeye sasa ni mstaafu aliyeitumikia nchi yake kwa muda mrefu na
nafasi mbalimbali. Ni vema sasa akatoa fursa kwa viongozi wengine walioko
madarakani kutimiza wajibu wao wa kuwatumikia watanzania. Muda wake umekwisha
na sasa ni busara akakaa kimya na kuchunga maneno yake.
Raisi mstaafu wa awamu
ya tatu mh. Benjamin William Mkapa aliwahi kusema (nanukuu):-
"Siku moja mtoto mdogo aliwahi kuniuliza. Nani ni bingwa wa
kuendesha shughuli za serikali? Nikatafakati sana swali lile, kisha baada ya
muda nikamjibu…Ni mwanasiasa aliyestaafu kisha akachunga ulimi wake…"
MWISHO
Tunamshauri ndugu Membe
kuuchukua ushauri huu wa Raisi mstaafu Benjamin Mkapa, utamsaidia. Aidha
tunamtaka afahamu kwamba watanzania wana imani kubwa na juhudi zinazofanywa na
serikali katika kupunguza matumizi, kuziba mianya ya rushwa, ukwepaji kodi na
ubadhirifu wa mali za umma. Wakati huu si wa kupika majungu, fitina wala
ubabaishaji. Ni wakati wa kuungana pamoja kama taifa na kuchapa kazi tu.
Asanteni.
Imetolewa na ndugu
ALLY S. HAPI
KATIBU WA IDARA,
ELIMU, UTAFITI NA
UONGOZI,
SHIRIKISHO LA VYUO VYA
ELIMU YA JUU TANZANIA
Ally S. Hapi, Katibu Wa Idara,
Elimu, Utafiti Na Uongozi,
No comments:
Post a Comment