Katika
utaratibu wake wa kujipanga na kuendelea kutekeleza mikakati ya malengo ya muda
mfupi na muda mrefu kwa ajili ya kufikia lengo kuu la kushinda uchaguzi,
kushika dola na kuongoza serikali kwa ajili ya kuwatumikia wananchi, Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimekuwa na utamaduni wa kuwa na vikao vya
kujitathmini na kufanya uchambuzi kila baada ya uchaguzi mkuu na kuweka mpango
kazi unaopaswa kutekelezwa na chama kwa miaka mitano inayofuata.
Vikao vya namna hiyo pia vimekuwa vikifanyika kila mwanzoni mwa mwaka mpya,
lengo kubwa likiwa ni kufanya tathmini na uchambuzi wa utekelezaji wa mpango
kazi huo na kuweka mikakati ya utekelezaji wa vipaumbele kwa mwaka mpya husika
kulingana na mpango huo.Mapendekezo ya vikao hivyo vya kiuchambuzi na tathmini (retreats) huwasilishwa kwenye vikao vya kikatiba vya chama kwa ajili ya kujadiliwa na kufanyiwa maamuzi kwa ajili ya utekelezaji wake kadri inavyoelekezwa na vikao husika katika ngazi mbalimbali za chama.
Ni vikao vya namna hii ambavyo huwakutanisha viongozi wa kisiasa, watendaji na wataalam wa masuala mbalimbali, vimekuwa moja ya nguzo muhimu za CHADEMA katika kujipanga na kuweka mikakati ya kukisuka na kukiimarisha chama kwa ajili ya kutekeleza lengo kuu la kushika dola kwa kuiondoa CCM madarakani na hatimaye kuwaongoza Watanzania kufikia matamanio ya MABADILIKO YA KWELI nchini, badala ya ‘cosmetic changes’ kama inavyofanyika sasa chini ya CCM.
Katika utaratibu huo huo ambao umeshakuwa ni utamaduni wa CHADEMA kwa miaka mingi sasa, vikao hivyo vinaendelea kufanya tathmini na uchambuzi wa mpango kazi wa mwaka 2010-2015 na kupanga kwa ajili ya 2016-2020 na kupendekeza kwa ajili ya 2016 kabla ya kuwasilisha kwenye vikao vya maamuzi kwa mwaka huu, ambavyo vitakaa kulingana na utaratibu wa kikatiba.
Ufafanuzi unaotolewa kupitia taarifa hii, utasaidia kusahihisha habari ambazo hazina ukweli zinazolenga kupotosha umma, zinazoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini kwa makusudi au kwa kutokujua taratibu za CHADEMA katika kupanga na kuendesha mambo yake.
Imetolewa leo Alhamis, Januari 7, 2016 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
CHADEMA
No comments:
Post a Comment