Na Nyakongo Manyama-MAELEZO
TAASISI ya watu wenye ulemavu wa
ngozi mkoa wa Dar es salaam inatarajia kufanya uzinduzi wa ‘stika’ maalum
yenye ujumbe wa kutokomeza mauaji ya watu wenye albinism utakaofanyika januari
26 mwaka huu.Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa taasisi hiyo Bw. Michael Lugendo amesema kuwa uzinduzi huo
utafanyika katika kituo cha polisi kati jijini Dar es Salaam kuanzia saa tano
asubuhi.
Bw. Michael Lugendo amesema kuwa stika
hiyo ina lengo la kuhamasisha jamii kuungana na Rais Mhe.Dkt. John Pombe
Magufuli na Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam ili kuyafanya mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi yatokomezwe na yabaki kuwa historia.
Kwa upande mwingine Bw. Lugendo
ameongeza kuwa kulingana na kasi ya mabadiliko tabia nchi, jamii isipochukua
hatua za makusudi kuna uwezekano wa watu wenye ulemavu wa ngozi kuangamizwa na
saratani ya ngozi.
Alisema watu wenye ulemavu wa ngozi
wanaishi katika mazingira ya umaskini kiasi kwamba waliowengi hawana uwezo wa
kupata fedha ya kununua mafuta ya kuzuia mionzi ya jua ambayo husababisha
saratani ya ngozi.“Sisi watu wenye ulemavu wa ngozi ni wahanga wakubwa sana na
jamii isipochukua hatua za makusudi upo uwezekano wa kuangamizwa na saratani ya
ngozi ukizingatia kwamba tunaishi katika mazingira ya umaskini na walio wengi
hatuna uwezo wa kupata fedha ya kununua mafuta” alisema Bw. Lugendo.
Aidha Bw. Lugendo amesema kuwa
taasisi hiyo imemteua Bw. Mbwana Ally Samata kuwa balozi wa kudumu wa kusemea
watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alibainisha kuwa majukumu ya Nahodha
huyo wa Timu ya Taifa ya Tanzania kwa ujumla ni kuhamasisha dunia kwa njia ya
soka kuhakikisha kwamba hakuna mlemavu wa ngozi anayefariki kwa kifo cha
saratani ya ngozi au mauaji ya kukatwa viungo yanayotokana na Imani za
kishirikina.
Bw. Lugendo aliwataka wadau mbalimbali,
kampuni, balozi mbalimbali, Mashirika yasiyokuwa ya Serikali kujitokeza ili
kuwezesha kutimiza lengo hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu dhidi ya watu wenye
ulemavu wa ngozi kupitia vyombo vya habari pamoja na jeshi la polisi.
No comments:
Post a Comment