JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA
KURUGENZI YA
MAWASILIANO YA RAIS IKULU
Simu: 255-22-2114512,
2116898
E-mail:
press@ikulu.go.tz
Tovuti : www.ikulu.go.tz
Faksi: 255-22-2113425
|
OFISI YA RAIS,
IKULU,
1 BARABARA YA BARACK OBAMA,
11400 DAR ES SALAAM.
Tanzania.
|
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 21 Januari, 2016 amewasili Mkoani Arusha ambapo keshokutwa tarehe 23
Januari, 2016 atatunuku kamisheni kwa maafisa wanafunzi wa kundi la 57/15
katika chuo cha mafunzo ya kijeshi (TMA) Monduli mkoani hapa.
Rais Magufuli amewasili Mjini Arusha akitokea Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) alikotua kwa ndege akitokea jijini Dar es salaam
na kupokelewa na mamia ya wananchi.
Akiwa uwanjani hapo Rais Magufuli amewashukuru wananchi kwa mapokezi
makubwa aliyoyapata na amewaeleza kuwa uchaguzi umekwisha, kilichobaki ni kazi
tu."Nawashukuru sana ndugu wananchi kwa mapokezi haya makubwa, naomba
kuwahakikishia kuwa uchaguzi umekwisha na sasa kilichobaki ni kuchapa kazi tu"
Alisema Rais Magufuli.
Akiwa njiani kutoka uwanja wa ndege wa KIA, Rais Magufuli amesimamishwa
na wananchi wa njiapanda ya KIA, Kikatiti, Usa River, Tengeru na Mount Meru
Mjini Arusha ambapo huko kote pamoja na kusisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na
kilichobaki ni kuchapa kazi, amewahakikishia kuwa hatawaangusha.
Dkt. Magufuli ametoa wito kwa watanzania kumuombea ili aendelee
kuwashughulikia wote wanaofanya ubadhilifu wa fedha za umma kupitia kampeni
yake ya kutumbua majipu.
"Nataka niwahakikishieni kuwa nitaendelea kutumbua majipu yote
mpaka yaishe, na naomba mniombee ili kazi hii ya kutumbua majipu ifanyike kwa
mafanikio" Alisisitiza Mheshimiwa Magufuli.
Aidha Rais Magufuli amesema tayari serikali imeanza kutoa fedha kwa
ajili ya kugharamia elimu ya Msingi na Sekondari baada ya kufuta ada na akaonya
kuwa watumishi wa umma hususani wakuu wa shule watakaothubutu kufanya
ubadhilifu wa fedha hizo watashughulikiwa.
Amesema yote aliyoyaahidi kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha na watanzania
kwa ujumla ikiwemo ujenzi wa barabara za Arusha, kulipa fidia za wananchi na
kufuta ada ya shule za msingi na sekondari yanatekelezwa.
Rais Magufuli amesisitiza kuwa serikali yake haitawabagua watanzania
kwa dini zao wala makabila yao na wala haitawabagua kwa milengo ya vyama vyao
na kanda zao na kuwataka watanzania wote kuiweka mbele Tanzania na
kushirikiana kuiendeleza.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha.
21 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment