JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
MAELEZO YA WAZIRI KUHUSU
TIBA ASILI NA TIBA MBADALA
Ndugu Wananchi, Katika nchi yoyote
ile uhuru usio na mipaka ni jambo la hatari; lakini pia hakuna haki isiyo na
wajibu. Vivyo hivyo, katika huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala hapa nchini
kuna Sheria, Kanuni na Taratibu za Maadili zinazoweka masharti, uhuru na
mipaka; pia haki na wajibu wa kila mdau.
Huduma za tiba asili
na tiba mbadala ni huduma zinazotambulika na Jamhuri yetu, watu wake na ina
thamani kubwa. Aidha, ni huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa.
Hata hivyo huduma hizo zimekumbwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuwepo kwa watoa huduma wasiozingatia Sheria, Kanuni na Miongozo
mbalimbali.
Kutokana na hali hiyo
na kutokana na ziara ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee
na Watoto, Mhe. Dkt. Hamisi A. Kigwangalla (Mb) kwa Tabibu Juma Mwaka Juma
tarehe 14/12/2015 na kufuatia uchambuzi uliofanywa na Wizara baada ya ziara hii,
Wizara imebaini changamoto zifuatazo:-
1. Huduma za tiba
asili na au tiba mbadala zinatolewa na watoa huduma wasiosajiliwa na Mamlaka
husika kwa mujibu wa Sheria. 2. Uwepo wa vituo vinavyotoa huduma za
Tiba Asili na au Tiba Mbadala bila kusajiliwa kwa mujibu wa Sheria.
3. Kutolewa dawa kwa
wagonjwa bila dawa hizo kusajiliwa na mamlaka husika. 4. Uingizaji na
matumizi ya vifaa vya uchunguzi ambavyo havijasajiliwa na mamlaka zinazohusika,
na
5. Utoaji wa
matangazo bila ya kufuatwa kwa matakwa ya sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.
Aidha baadhi ya matangazo hayo yamekuwa na taarifa zinazoweza kuleta madhara na
kupotosha Umma wa Watanzania.
Ndugu Wananchi,
Kutokana na hali hiyo, Wizara itahakikisha kuwa huduma za tiba asili na tiba mbadala zinatolewa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo. Lengo ni kuwezesha huduma za tiba asili na tiba mbadala zinakuwa huduma rafiki na salama kwa watumiaji. Tunao wajibu wa kuwalinda wananchi, vile vile tunaowajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala ili kufanya shughuli zao vizuri.
Hivyo kwa upande wetu
Wizara itahakikisha kuwa:- 1. Baraza na sehemu inayosimamia huduma
za Tiba Asili na Tiba Mbadala inakuwa na watumishi wa kutosha kwa mujibu wa
Ikama. 2. Kunakuwa na Mpango Mkakati wa muda mrefu kuwezesha kufanikisha
uboreshaji wa huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.3. Watoa huduma wote,
vituo vyote vya kutolea huduma, dawa na vifaa na vifaa tiba vinavyotumika
vinasajiliwa. 4. Utaandaliwa mwongozo wa mafunzo kwa watoa huduma wote nchini,
kuhusu namna ya kuweka kumbukumbu za wagonjwa, kutoa rufaa kwa wagonjwa na
kutengeneza dawa zilizo bora. 5. Kunakuwa na mawasiliano na Wizara
zinazohusika na habari na mawasiliano ili kuboresha utoaji matangazo yanayohusu
Tiba Asili na Tiba Mbadala. 6. Kunakuwa na mawasiliano na Ofisi ya
Rais TAMISEMI na Taasisi za Utafiti ili kuboresha huduma za tiba asili na tiba
mbadala nchini. 7. Tutafanya mabadiliko ya Sheria ili kuongeza kiwango cha adhabu
kwa watakaokiuka, na pia tunakusudia kuondoa Kanuni inayoruhusu matangazo kwa
idhini ya Baraza kwa sababu inaweka mianya ya matumizi mabaya ya fursa ndogo ya
matangazo inayotolewa.
Ndugu Wananchi, Katika kufanikisha
hayo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa maelekezo
yafuatayo kwa watoa huduma na jamii:-1. Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kutoa huduma
za tiba asili na au tiba mbadala bila kusajiliwa. Ninalielekeza Baraza la Tiba
Asili na Tiba Mbadala kuhakikisha kuwa watoaji huduma wote wanasajiliwa kwa
mujibu wa Sheria: (a) Mijini, (Majiji, Manispaa na Miji) – usajili wao ukamilike
katika kipindi cha miezi mitatu; kuanzia Januari 15, 2016 na (b) Vijijini,
Halmashauri zote zilizobaki – usajili wao ukamilike katika kipindi cha miezi
sita kuanzia Januari 15, 2016. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa
kwa yeyote atakaye puuza kujisajili katika kipindi hicho 2. Hairuhusiwi kuuza
na au kugawa dawa yoyote ile ya tiba asili au tiba mbadala mpaka iwe
imesajiliwa na Baraza baada ya kuchunguzwa na Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu
wa Serikali kuwa ni salama na kupewa kibali na Mamlaka ya Chakula na Dawa
(TFDA). 3. Hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili na
au tiba mbadala bila kukisajili. 4. Wizara inapiga marufuku kwa mtu
binafsi au taasisi yoyote ile kutumia kifaa au kifaa tiba chochote bila
kukisajili TFDA na kupewa kibali; na 5. Matangazo yote yanayohusu Tiba Asili
na Tiba Mbadala ambayo hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia leo tarehe
15/1/2016. Wizara inavitaka vyombo vya Habari hasa Televisheni, Radio na
Magazeti kuzingatia Sheria na Kanuni za Tiba Asili na Tiba Mbadala inayozuia
matangazo ambayo hayajachunguzwa na Baraza. Ni wajibu wa vyombo vya habari
kujiridhisha na Mamlaka husika yaani Baraza kabla ya kutoa tangazo lolote
linalohusu Tiba Asili na Tiba Mbadala. Wizara itashirikiana na Mamlaka
zinazohusika na habari na mawasiliano kutekeleza agizo hili. Vile vile,
hairuhusiwi kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari na mikutano ya
hadhara kuhusu tiba asili na tiba mbadala.
Ndugu Wananchi, Katika kuwezesha
ulinzi wa afya za wananchi, kila mmoja wote alinde afya yake kwa kuhakikisha
kuwa huduma anayopata ya tiba asili na tiba mbadala ni kwa mujibu wa Sheria,
Kanuni na Miongozo inayotolewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto. Ni uhakika uliowazi kuwa kwa pamoja tukiboresha huduma za tiba
asili siyo tu tutaboresha afya zetu bali pia tutaweza kuuza dawa na huduma hizo
nje ya nchi na kupata fedha za kigeni kupitia na hivyo kuboresha uchumi wa mtu
mmoja mmoja, jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa pamoja
tushirikiane kuboresha huduma za tiba asili na tiba mbadala nchini.
INAWEZEKANA.
Ummy A. Mwalimu (Mb) WAZIRI WA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO 15 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment