Serikali imeahidi kuendelea na ujenzi
wa barabara katika maeneo tofauti nchini kwa kiwango cha lami ili kutatua adha
kubwa ya ubovu wa barabara ulipo katika maeneo mengi nchini.
Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Eng Godwin
Ngonyani akijibu maswali ya wabunge waliouliza kuhusu mpango wa serikali
kuboresha barabara zilizopo na kujenga mpya ili kukabiliana na adha ya ubovu wa
barabara nchini.
Akijibu swali la Mhe Richard Mganga
Ndassa Mbunge wa Sumve (CCM) lililohitaji ufafanuzi wa serikali ni
lini ujenzi wa barabara ya Magu-Bukwimba –Ngudu-Hungumalwa itajengwa kwa
kiwango cha lami, Mhe Eng Godwin Ngonyani amesema katika mwaka wa
fedha 2014/15 na 2015/16 serikali ilitenga jumla ya shilling millioni 200 kwa
ajili ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara hiyo yenye urefu wa
kilometa 70 na taratibu za kumtafuta Mhandisi Mshauri zinaendelea na baada ya
kukamilika kwa usanifu na kupata gharama za mradi huo, Serikali itatafuta fedha
za kuanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Aidha akijibu pia swali la Mhe Fredy
Atupele Mwakibete Mbunge wa Busokelo (CCM) aliyehitaji kujua ni lini
barabara ya Katumba-Mbambo-Tukuyu yenye urefu wa Kilometa 82 inayoanzia
Katumba(RDC) kupitia Mpombo,Kandete,Isange,Lwanga, Mbambo (BDC) hadi Tukuyu
(RDC) itajengwa kwa kiwango cha lami.
Akijibu swali hilo, Mhe. Eng Godwin
Ngonyani amesema kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS)
kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, katika mwaka wa fedha 2009//10 Serikali
ilianza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami na ambapo
upembuzi yakinifu na sanifu wa kina ulikamilika na baadae Serikali iliamua
kujenga kilometa 10 ambapo mwezi April,2014 Wakala wa Barabara na kampuni ya
CICO ilijenga barabara hiyo kuanzia Lupaso hadi Buseji,Wilayani Busokelo.
Serikali kupiti Wakala wa Barabara
(TANROADS) inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwangocha lami katika Kata,
Wilaya na Mikoa mbalimbali nchini ili kukabiliana na adha ya ubovu wa
barabara ambao umesababisha watu kukosa mawasiliano baina ya maeneo.
No comments:
Post a Comment