WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo kitovu cha nchi na kwamba kila Mtanzania ameelekeza jicho lake pale kwa sababu anasubiri kupata huduma ya msingi.
“Hapa ndiyo kitovu
cha nchi na Watanzania wote macho yao yako huku. Kwa nini? Kwa sababu huduma
zinasowagusa za barabara, maji, elimu, zinatokea huku kwa maana ya bajeti na
usimamizi,” alisema.
Ametoa kauli hiyo leo
(Alhamisi, Januari 21, 2016) wakati akizungumza na wakurugenzi, wakuu wa
taasisi na watumishi wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwenye mkutano uliofanyika
ofisi ya TAMISEMI mjini Dodoma.
“Wananchi
wakilalamikia ukosefu wa hizi huduma chanzo ni hapa. Katika wizara kuna
mawaziri lakini wao kule ni wasimamizi wakuu. Ninyi chini yenu kuna mikoa,
wilaya, halmashauri, rasimali watu na raslimali fedha za kuwasaidia kufikisha
huduma tarajiwa kwa Watanzania walio wengi,” alisisitiza.
Waziri Mkuu ameitaka
ofisi hiyo ihakikishe inaisimamia vizuri mikoa na halmashauri ili Serikali
iweze kupata matokeo mazuri na tarajiwa.
Waziri Mkuu alisema
jukumu kubwa lililopo hivi sasa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ni
kuhakikisha kuwa zinabuni vyanzo vipya vya mapato na kusimamia vizuri
ukusanyaji wa mapato ya serikali.
“Hatukubaliani na
uzembe kwenye idara na halmashauri za wilaya kwa kuwa hivi sasa Serikali ya
Awamu ya Tano inasimamia utumishi uliotukuka na wenye uadilifu hivyo kila mmoja
ahakikishe anasimamia vizuri eneo lake,” alisema.
Alisema Serikali ya
Awamu ya Tano imekusudia kuwahudumia ipasavyo Watanzania wenye uelewa tofauti
na matakwa tofauti na kwa kuanzia Serikali imeanza kuwajenga watumishi wa
Serikali kutambua kuwa wao ni wahudumu wa wananchi hivyo inawapasa kuwahudumia
vema.
“Lazima tujenge moyo
wa huruma wa kuwahudumia wenzetu, anapokuja mwananchi msikilize, mhudumie na
mwelekeze eneo sahihi ili aweze kupata huduma. Lazima tusimamie na kuona maeneo
yote yanafanya kazi kama ilivyokusudiwa, ili kupata matokeo tarajiwa iwe ni
wajibu ya kila mmoja kuhakikisha kuwa anatoa usimamizi thabiti katika eneo
lake,” alisisitiza.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza na watumishi hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –
TAMISEMI, Bw. George Simbachawene alisema TAMISEMI wapo tayari kubadilika na
kufanya kazi kama kauli ya Rais John Pombe Magufuli inavyotaka, yaani HAPA KAZI
TU.
Naye, Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Bernard Makali alimpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa
kusimamia vizuri masuala ya elimu nchini wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI
anayeshughulikia masuala ya elimu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, JANUARI 21,
2016.
No comments:
Post a Comment