Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue akifafanua moja ya swali lililoulizwa kutoka kwa mmoja Waandishi wa habari (hayupo pichani) kuhusiana na suala zima la kusimamishwa kwa Mkurugenzi wa NIDA,katika mkutano na waandishi wa habari, uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam mapema leo, kuhusu uamuzi wa Rais Magufuli kutengua uteuzi wa Mkurugenzi wa NIDA, Dickson Maimu.
Rais Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu
(pichani) kuanzia leo.
1.1 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, ametengua uteuzi wa Bwana Dickson E. MAIMU, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa kuanzia leo, tarehe 25 Januari, 2016.
1.2 Aidha, baada ya utenguzi huo, Bwana Dickson E. MAIMUamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi, pamoja na wafuatao:
1.2.1 Bwana Joseph MAKANI, Mkurugenzi wa TEHAMA
1.2.2. Bi Rahel MAPANDE, Afisa Ugavi Mkuu
1.2.3 Bi Sabrina NYONI, Mkurugenzi wa Sheria
1.2.4 Bwana George NTALIMA, Afisa usafirishaji
1.3 Taarifa zilizomfikia Rais zinaonesha kuwa NIDA hadi sasa imetumia Sh.179.6 bilioni. Kiasi hiki ni kikubwa na Rais angependa ufanyike uchunguzi na ukaguzi jinsi fedha hizi zilivyotumika, maana Rais amekuwa akipokea malalamiko ya wananchi kuhusiana na kasi ndogo ya utoaji wa Vitambulisho vya Taifa.
1.4 Hivyo, Rais ameelekeza Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) wafanye ukaguzi maalum wa manunuzi yote yaliyofanywa na NIDA.
1.5 Rais pia ameelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali afanye ukaguzi maalum wa hesabu za NIDA, ikiwemo ukaguzi wa “value for money” baada ya kuthibitisha idadi halisi ya vitambulisho vilivyotolewa hadi sasa.
1.6 Rais vile vile ameelekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ifanye uchunguzi kujiridhisha kama kulikuwa na vitendo vya rushwa au la.
2.0 Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa
2.1 Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwenye Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Mahadhi Juma MAALIM ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Kuwait, kufuatia uamuzi wa Serikali kufungua Ofisi ya Ubalozi katika nchi hiyo rafiki.
2.2 Rais ameagiza Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kianda na Kimataifa kuwarejesha nyumbani mara moja Mabalozi wawili ambao mikataba yao imeisha. Leo hii Mabalozi hao wanatakiwa kukabidhi kazi kwa Afisa Mkuu au Mwandamizi aliye chini yao. Mabalozi hao ni:
2.2.1 Bi Batilda Salha BURIANI, aliyeko Tokyo, Japan
2. 2.2 Dkt. James Alex MSEKELA, aliyeko Rome, Italia.
2.3 Rais amemrejesha nyumbani Balozi wa Tanzania aliyeko London, Uingereza, Bwana Peter Allan KALLAGHE. Anarejea Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa atakapopangiwa kazi nyingine.
2.4 Kwa maana hiyo, vituo vya Ubalozi vifuatavyo viko wazi:
2.4.1 London, kufuatia kurejea nchini kwa Balozi Peter A. KALLAGHE
2.4.2 Brussels, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Deodorous KAMALAkuchaguliwa kuwa Mbunge.
2.4.3 Rome, Italia, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Dkt. James Alex MSEKELA.
2.4.4 Tokyo, Japan, kufuatia kuisha kwa mkataba wa Bibi Batilda BURIANI
2.4.5 Kuala Lumpar, Malaysia, kufuatia aliyekuwa Balozi, Dkt. Aziz Ponray MLIMA, kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Afrika Mashariki na Ushirikiano wa Kikanda na Kimataifa.
2.4.6 Brasilia, Brazil, kufuatia kustaafu kwa aliyekuwa Balozi, Bwana Francis MALAMBUGI.
3.0 Tawala za Mikoa
3.1 Rais ametengua uteuzi wa Eng. Madeni Juma KIPANDE kabla hajathibitishwa kwenye cheo cha Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi kutokana na utendaji kazi usioridhisha.
4.0 Utumishi wa Umma
3.2 Nachukua nafasi hii kuwahimiza viongozi wote katika Utumishi wa Umma, na watumishi wote wa umma, kubadilika kwa dhati kwenye utendaji wao na uadilifu wao.
3.3 Napenda kusisitiza kuwa Rais na sisi tunaomsaidia hatuoni raha kuchukua hatua dhidi ya viongozi na watumishi wengine. Tungependa kila mtu mwenyewe ajirekebishe na kutomfikisha Rais mahali ambapo inabidi amchukulie hatua. Mambo yafuatayo ni muhimu:
4.2.1 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu isipate kigugumizi kusimamia utendaji na maadili ya kazi.
4.2.2 Kila kiongozi na kila mamlaka ya nidhamu asipate kigugumizi kuchukua hatua za nidhamu, lakini afanye hivyo kwa kuzingatia kwa ukamilifu sheria, kanuni na taratibu katika Utumishi wa Umma.
4.2.3 Lazima uongozi na watumishi wa umma wawahudumie wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na heshima. Kwa sababu hiyo:
a) Kila ofisi ya Serikali iwe na dawati la kusikiliza shida za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.
b) Kwenye kila Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wajenge uwezo wa kushughulikia shida za wananchi kwa ukamilifu na kwa wakati. Kwa muundo wa Serikali yetu hakuna sababu kwa mwananchi kufunga safari mpaka Ikulu Dar es Salaam kwa kuamini kuwa ni Rais tu anayeweza kumaliza matatizo yake, maana wawakilishi wa Rais wako kila pembe ya nchi yetu. Ikibidi wananchi wafike Ikulu ina maana hao wawakilishi wa Rais hawakutimiza wajibu wao.
c) Kuanzia sasa watumishi wote wa umma wavae majina yao ili iwe rahisi kwa mwananchi kumtambua anayemhudumia na hivyo kumsifu mtumishi wa umma anayewahudumia kwa weledi, uaminifu na kwa wakati, na kumtolea taarifa yule anayefanya mambo ya hovyo.
d) Kila ofisi ya Serikali iwe na utaratibu wa kupokea maoni ya wananchi kuhusu huduma inayotolewa kwenye ofisi hizo, na kushughulikia haraka maeneo yote ambayo wananchi wataonesha kutoridhika na huduma.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
25 Januari, 2016
No comments:
Post a Comment