Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Mahakama Kuu ya Tanzania Bw.
Nurdin Ndimbe (kushoto) akiagana na Afisa Mfawidhi wa Mahabusu ya Watoto ya jijini Dar es salaam Bw. Ramadhan Yahaya (kulia) mara baada ya kutoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Nurdin Ndimbe (kushoto) akimkabidhi Afisa Mfawidhi wa Mahabusu ya Watoto jijini Dar es salaam Bw. Ramadhan Yahaya (kulia) msaada wa vyakula na vitu mbalimbali vilivyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania leo.
Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Mahakama Kuu ya Tanzania Bw. Nurdin Ndimbe (kushoto) akishirikiana na Afisa Mfawidhi wa Mahabusu ya Watoto jijini Dar es salaam Bw. Ramadhan Yahaya (kulia) kupakua msaada wa vyakula na vitu mbalimbali vilivyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania leo.
Na. Aron Msigwa-MAELEZO.
Jamii imeaswa kujenga
utamaduni wa kuwasaidia watu na makundi yenye mahitaji maalumu hususan wafungwa
walio magerezani na wasiojiweza ili kudumisha upendo na kuyafanya makundi
hayo kujiona yanathaminiwa katika jamii.
Wito huo umetolewa leo
jijini Dar es salaam na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Mahakama Kuu
ya Tanzania Bw. Nurdin Ndimbe wakati akikabidhi msaada wa vyakula na vitu
mbalimbali kwa Mahabusu ya Watoto ya jijini Dar es salaam vilivyotolewa na
Mahakama Kuu ya Tanzania kama zawadi yao ya mpya 2016..
Bw. Ndimbe amesema
Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa msaada wa vitu mbalimbali vikiwemo Mchele,
Sabuni, Vinywaji, Chumvi, Unga wa Ngano, Unga wa Sembe, Mchele ,Sukari na
Mafuta ya kupikia kwa Mahabusu hao kuonyesha Upendo na namna Mahakama
hiyo inavyowathamini watoto hao.
Ameongeza kuwa Mahakama
Kuu ya Tanzania imetoa msaada huo kwa lengo la kujenga mahusiano mema baina
yake na watoto hao ili waendelee kuipenda na kuwa na mtazamo chanya juu ya
utendaji wake.
‘ Nimekuja kukabidhi
msaada huu kwa niaba ya Mahakama Kuu ya Tanzania kwa Mahabusu hii ya Watoto
ikiwa ni zawadi yao ya mwaka mpya, lengo letu ni kujenga mahusiano mema kati
yetu Mahakama na watoto hawa wajue kuwa tunasaidia jamii katika masuala
mbalimbali’’ Amesema Bw. Ndimbe.
Kwa upande wake Afisa
Mfawidhi wa Mahabusu hiyo Bw. Ramadhan Yahaya akizungumza mara baada ya kupokea
msaada huo ameishukuru Mahakama Kuu ya Tanzania kwa uamuzi wake wa kuwakumbuka
Mahabusu hao.
Amesema kitendo cha
Mahakama Kuu ya Tanzania kuwapatia msaada huo kimewapa faraja watoto hao na
kuwafanya wajione wanathaminiwa na kupendwa na Mahakama hiyo.
Ametoa wito kwa Taasisi
na Mashirika mengine kuiga mfano huo ulioonyeshwa na Mahakama Kuu
ya Tanzania ili kudumisha upendo miongoni mwa makundi ya watu wenye mahitaji
maalum.
No comments:
Post a Comment