Makamu wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa
Balozi Seif Ali Idd amemhakikishia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.
John Pombe Magufuli kuwa hali ya Zanzibar ni shwari na Wazanzibar wanasubiri
kutangaziwa tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi.
Balozi Seif Ali Idd ameyasema hayo Ikulu jijini Dar es salaam
leo tarehe 20 Januari, 2016 mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na
Rais Magufuli.
"Mimi nimekuja kumpa taarifa juu ya hali yetu Zanzibar
inavyokwenda, nimemueleza kwamba Zanzibar ipo salama, Zanzibar ina utulivu na
ina amani, nimeona nije nimueleze kwa kuwa yeye ni kiongozi wetu"alisisitiza Balozi Seif Ali Idd.
Makamu huyo wa pili wa Zanzibar ameongeza kuwa kutokana na uwepo
wa amani na utulivu, wananchi wa Zanzibar wanaendelea na shughuli zao kama
kawaida tofauti na inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
"Hayo yanayoandikwa kwenye magazeti kuwa Zanzibar kuna
fujo, Zanzibar kutatokea machafuko sio kweli, na kama unavyojua uchaguzi
ulifutwa na tume ya uchaguzi na tunasubiri tarehe mpya ya uchaguzi itangazwe na
tume ili tufanye uchaguzi" amebainisha Balozi Seif Ali Idd.
Gerson Msigwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU.
Dar es salaam.
No comments:
Post a Comment