SHIRIKA LA Majisafi na Majitaka Dar es salaam
(DAWASCO), imetangaza kuwapo tatizo la upatikanaji wa huduma ya Maji katika
maeneo yote yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu chini ya jiji la Dar es salaam,
pamoja na baadhi ya maeneo ya mji wa Bagamoyo mkoani Pwani kutokana
na mtambo huo kuzimwa kwa wastani wa saa 48 kuanzia siku ya Jumamosi 23/01/2016
hadi Jumapili 24/01/2016.
Taarifa ya kwa vyombo vya habari iliyosainiwa
na kaimu meneja uhusiano wa DAWASCO, Bi Everlasting Lyaro, imeeleza kuwa sababu ya
kuzimwa kwa mtambo huo, ni kuruhusu mkandarasi kuunganisha bomba jipya na bomba
la zamani katika tanki la Maji wazo-Tegeta, zoezi ambalo linaashiria kukamilika
kwa upanuzi wa mtambo wa Ruvu Chini, hivyo kuondoa tatizo la upatikanaji wa huduma ya Maji katika
maeneo yanayohudumiwa na mtambo wa Ruvu chini.
“Tunaelekea kwenye hatua za mwisho za kupokea
Maji mengi kutoka mtambo wa Ruvu Chini baada ya kazi ya upanuzi inayoelekea
kukamilika mapema mwezi February mwaka huu, na kiasi cha Maji kitaongezeka
kutoka wastani wa Lita Milioni 182,000 zinazozalishwa sasa hadi Lita Milioni
270,000. Hivyo kuzimwa kwa mtambo huu ni moja ya hatua za mwisho-mwisho katika
ukamilishaji wa Mradi wa Ruvu Chini” alisema Lyaro
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, DAWASCO imetoa
wito kwa wateja na wananchi wote kuhifadhi Maji ya kutosha na kuyatumia kwa
matumizi muhimu ili kukidhi mahitaji husika kwa kipindi hicho chote.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa matengenezo hayo
yatasababisha maeneo mengi ya jiji la Dar es salaam kukosa Maji, pamoja na mji
wa Bagamoyo vijiji vya Zinga, Kerege na Mapinga, Bunju, Boko, Tegeta, Kunduchi,
Salasala, Jangwani, Mbezi Beach na Kawe.
Maeneo mengine ni Mlalakuwa, Mwenge,
Mikocheni, Msasani, Sinza, Kijitonyama, Kinondoni, Oysterbay, Kigogo,
Mburahati, Hospitali ya Rufaa Muhimbili, Buguruni, Chang’ombe na Keko.
No comments:
Post a Comment