Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Faustin
Kamuzora alifanya ziara ya kutembelea Shirika la Posta Tanzania ili kufahamu
utendaji kazi na utekelezaji wa majukumu ya Shirika.
Katika ziara hiyo
Prof. Kamuzora aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Dkt. Maria Sasabo na
kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Shirika hilo. Katika ziara hiyo Prof.
Kamuzora alimuagiza Kaimu Posta Masta Kuu wa Shirika la Posta Tanzania
Ndugu Fortunatus Kapinga kuhakikisha kuwa ukusanyaji wa mapato yote
ya Shirika la Posta Tanzania (TPC) nchi nzima yanafanyika kwa kutumia njia ya
elektroniki ambapo alisema kuwa, “Shirika liboreshe mifumo yake ya
kielektroniki ili kupunguza mianya ya wizi na upotevu wa fedha za Shirika na
kufanikisha ongezeko la ukusanyaji wa mapato ya Serikali”.
Prof. Kamuzora
aliongeza kuwa Shirika la Posta Tanzania liendane na mabadiliko ili liende
kuwahudumia wananchi wa sasa na wa vizazi vijavyo. Shirika ni la kipekee na
lina nafasi nzuri ya kutoa huduma kwa wananchi kama ambavyo Shirika kama hili
linafanya kazi nzuri kwenye nchi ya China na Brazil.
Aidha, Prof. Kamuzora
aliwaagiza Viongozi wa wasimamizi wa Shirika la Posta Tanzania kutumia Sheria,
Kanuni na taratibu za kuwasimamia wafanyakazi na kuwachukulia hatua kali na za
kinidhamu watumishi wazembe; wasiotimiza majukumu yao; wasio waaminifu na
wabadhirifu. Aliongeza kuwa watendaji wafanye kazi na kusimamia Shirika kwa
kuwekeana malengo kama inavyojulikana kisheria kwa kutumia Mfumo wa wa Wazi wa
Upimaji Utendaji Kazi (OPRAS). Alisisitiza kuwa, “Sheria zilizopo zinatosha
kumsimamisha mtumishi kazi kwa makosa na hatimaye kumfukuza kazi kwa kuwa
watumishi wazembe na wasio waadilifu wanawafanya wananchi wawe na mtazamo hasi
na Serikali yao”.
Prof. Kamuzora
alisema kuwa wateja wanahitaji huduma nzuri; ya uhakika na kufikishiwa
vifurushi, barua, vipeto na bidhaa nyingine kwa wakati. Aliwaagiza viongozi wa
Shirika kuangalia uwezekano wa kupunguza gharama za uendeshaji ili kuendesha
Shirika kwa tija na faida. Prof. Kamuzora alisema, “Uchumi wa nchi hauwezi
kukua wala kwenda popote bila kufanya kazi kwa tija. Alivitaka vyama vya
wafanyakazi visiwatetee watumishi wazembe na vishirikiane na Serikali
kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika na watumie mtandao mpana wa
Shirika uliopo nchi nzima na kuangalia fursa zilizopo ili kufikisha huduma kwa
wateja.
Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo anayeshughulikia Mawasiliano ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wake
Dkt. Maria Sasabo aliagiza kuwa, “Shirika lijipange haraka na kuongeza kasi ya
utendaji kazi ya kuwahudumia wateja wake na wananchi ili kuweza kuendana na
Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli”. Dkt. Maria Sasabo aliongeza kuwa Shirika la Posta lipo
nchi nyingi duniani na bado linahitajika hivyo ni muhimu kujipanga kuendana na
mahitaji ya sasa ya wateja na Shirika libadilishe utaratibu wa utendaji kazi na
kuondoa urasimu ili kuweza kuwahudumia wateja. Dkt. Maria Sasabo aliwaagiza viongozi
wa Shirika wafanye tathmini na kuangalia namna bora ya kujiendesha ikiwemo
kupitia upya muundo na majukumu ya Shirika.
Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo anayeshughulikia Mawasiliano Prof. Kamuzora aliuagiza uongozi wa Shirika
la Posta Tanzania kuongeza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa
kuwa na huduma za ziada za kisasa zinazoendana na mahitaji ya wateja kwa
kutumia biashara mtandao kusafirisha na kufanikisha usambazaji wa huduma na
bidhaa za wateja kama vile uagizaji wa magari; vitabu na bidhaa nyingine kwa
kushirikiana na kampuni kubwa duniani kama vile Alibaba, Amazon na eBay.
No comments:
Post a Comment