Monday, January 25, 2016

TAMKO KUHUSU MWENENDO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU NCHINI LILILOTOLEWA NA MHE. UMMY MWALIMU (MB); WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO, TAREHE 25 JANUARI 2016

Wizara yangu inaendelea kutoa taarifa ya wiki kwa umma kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu hapa nchini. Hadi kufikia tarehe 24 Januari 2016, jumla ya watu 14,608 wameugua ugonjwa huo, na kati yao watu 228 wamepoteza maisha kwa ugonjwa huu. Njombe, Ruvuma na Mtwara ndiyo Mikoa pekee ambayo haijawahi kuripoti mgonjwa yoyote wa kipindupindu, tangu mlipuko huu uanze mnamo mwezi Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa Takwimu za kuanzia tarehe 18 hadi 24 Januari 2016, ni kuwa jumla ya Mikoa ambayo imeripoti kuwa na wagonjwa ni 15 ambapo idadi ya wagonjwa 524 na vifo 10 vimeripotiwa. Idadi ya wagonjwa walioripotiwa wiki hii imepungua ukiliinganisha na idadi ya wiki iliyoishia tarehe 17 ambapo kulikuwa na wagonjwa 621 na vifo 14 ambalo ni punguzo la asilimia (16%). Mkoa wa Morogoro bado umeendelea kuripoti idadi kubwa zaidi ya wagonjwa ukilinganishwa na Mikoa mingine, (Manispaa ya Morogoro 89, Halmashauri ya Morogoro 36, Mvomero 17), ukifuatiwa na mikoa ya Mwanza (Ukerewe 36, Nyamagana 19 na Ilemela 13), Simiyu (Bariadi DC 29 na Bariadi municipal 23), Manyara (Simanjiro 48), Mara (Musoma Manispaa 11, Musoma DC 8, Rorya 8 na Butiama 8), Geita (Geita DC 21 na Geita TC 6)  na Mbeya (Kyela 26).
Mikoa mingine ambayo bado pia imeendelea kuripoti wagonjwa ni pamoja na Dodoma (Wagonjwa 22), Arusha (21), Tabora (18), Singida (18), Lindi (12), Rukwa (7), Kilimanjaro (6) na Kagera (2).

Ndugu Waandishi wa Habari,
Mwanzoni mwa mwezi Januari mwaka huu, Wizara yangu kwa kushirikiana na wadau ilituma timu ya jopo la wataalam kutoka ngazi ya Taifa kwenda kusaidiana na wataalam waliopo katika ngazi ya mkoa na halmashauri katika mikoa 7 iliyokuwa inatoa taarifa ya kuwa na  wagonjwa wengi zaidi. Mikoa hiyo ni Arusha, Manyara, Mwanza, Simiyu, Singida, Mara na Morogoro. Mafanikio ya kazi iliyofanywa na Jopo hilo yameanza kuonekana kwani katika Mikoa hiyo saba idadi ya wagonjwa wa kipindupindu imeanza kupungua. Pamoja na mafanikio hayo zipo changamoto ambazo timu hizo ilizibaini kuwepo ambazo zinachangia kulegalega kwa juhudi za kupambana na Kipindupindu nazo ni;
  1. Kuwepo na idadi ndogo ya kaya ambazo zinamiliki na kutumia vyoo bora hususani katika maeneo ambayo yameathirika zaidi na ugonjwa huu.
  2. Kutokuwepo kwa miundombinu stahiki ikiwemo vyoo na maji katika Maeneo ya mikusanyiko kama masoko na minada kutokuwa na
  3. Wananchi kutokutii sheria zilizopo kwa kuendelea kuuza chakula bila kuzingatia kanuni za afya na kuuza matunda yaliyokwisha katwakatwa maeneo yasiyo salama.
  4. Utiririshaji wa maji taka kwenye vyanzo vya maji, pamoja na kujisaidia maeneo ya wazi na pembezoni karibu na vyanzo vya maji.
  5. Kuwepo kwa idadi ndogo ya watu wanaopata maji safi na salama ya kunywa. Aidha utakasaji wa maji katika ngazi ya kaya kwa kuyachemsha au kwa kutumia vidonge vya kutakasia bado ni changamoto kubwa.
  6. Wagonjwa wa Kipindupindu kuchelewa kufika Kambi za Matibabu.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kutokana na changamoto hizo, napenda kuikumbusha jamii kuwa kipindupindu ni ugonjwa unaochochewa na mazingira machafu ikiwemo ukosekanaji wa vyoo na hivyo kuletea vinyesi vyenye vimelea kuwa chanzo kikuu cha maambukizi, utiririshaji wa maji taka na vinyesi ambao unaweza kupelekea kuchafuka kwa vyanzo vya maji,  kutokuzingatia kanuni za afya wakati wa utayarishaji wa vyakula na matunda, Kula vyakula au vinywaji au pombe za kienyeji zisizoandaliwa kwa kufuata kanuni za afya na kugusa matapishi ya mgonjwa wa kipindupindu au kwenye kitu chochote kilichochafuliwa na kinyesi au matapishi ya mgonjwa.

Ndugu Waandishi wa Habari,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inaendelea kusisitiza kwa jamii kuzingatia yafuatayo:
-      Kunywa maji yaliyo safi na salama.
-      Kuepuka kula chakula kilichoandaliwa katika mazingira yasiyo safi na salama.
-      Kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka hasa kabla ya kula na baada ya kutoka chooni.
-      Kutumia vyoo wakati wote na kutokujisaidia ovyo katika vyanzo vya maji vya mito, maziwa na mabwawa.
-      Kutokutiririsha maji taka na vinyesi ili kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji.

Wananchi wanaombwa kuwahi mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili kuu za ugonjwa wa kipindupindu kwani Mgonjwa anaweza kupoteza maisha endapo hatapata huduma yoyote ya tiba katika muda mfupi na hasa kutokana na kuishiwa maji. Dalili hizo ni pamoja na  kuanza ghafla kuharisha mfululizo kinyesi cha majimaji meupe kama maji yaliyooshea mchele na kinaweza kuambatana na kutapika, kulegea, kusikia kiu, midomo kukauka, na kuishiwa nguvu.



Ndugu Waandishi wa Habari,
Napenda kurudia tena kutoa agizo kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri pamoja na watendaji wake kote  nchini kuendeleza juhudi za kuzuia kusambaa kwa mlipuko ambazo ni pamoja na:
  • Uundaji wa Timu za Mikoa na Wilaya ambazo zitashirikisha kila sekta na wadau mbalimbali katika hatua mbalimbali za kuratibu mikakati ya udhibiti wa ugonjwa wa Kipindupindu.
  • Ushirikishwaji wa viongozi ngazi mbali mbali, hasa ngazi za Halmashauri kushirikisha madiwani na viongozi wa kata, vijiji, na mitaa hasa katika Kusimamia utekelezwaji wa Sheria ya Afya ya Mazingira na Sheria ndogo ndogo (By-Laws). Matumizi ya Sheria hizi pia yazingatie Haki za Binadamu hususan katika uamuzi wa kutumia nguvu ambayo inaweza kuleta madhara kwa mtu.
  • Ushirikishwaji wa wadau mbali mbali huko Mikoani, Wilayani na kwenye Halmashauri, ikiwemo Sekta Binafsi na Viongozi wa dini, katika jitihada za kupambana na Kipindupindu.
  • Mamlaka husika kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama ikiwa ni pamoja na uwekaji wa dawa ya klorini kwenye maji na kupima usalama wa maji mara kwa mara.
  • Watumishi wa Afya kuhakikisha wanafuatilia kwa karibu maeneo yote walikotoka wagonjwa ili kubaini chanzo na kuchukua hatua haraka.
  • Upatikanaji wa dawa za kutibu maji (Water Guard, Aqua Tabs) katika maeneo ya mlipuko.
  • Juhudi kubwa ziongezwe kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya vyoo bora kwa kila kaya.
  • Uelimishwaji wa Baba na Mama Lishe, na wauzaji wengine wa vyakula kuhusu kanuni za afya.
  • Uhamasishaji wa Wananchi wanaopata ugonjwa huu kutumia maji ya chumvi  chumvi (ORS) na kuripoti mapema katika vituo vya huduma.
  • Kila Halmashauri inapaswa kutoa taarifa mapema na kwa wakati bila kuficha pindi wanapopata wagonjwa wapya na jamii isiwekewe vikwazo vya faini au kunyanyapaliwa wapatapo ugonjwa huu kwani inaweza kusababisha wananchi kuogopa kwenda katika vituo vya afya.

Hitimisho:
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, inatoa rai kwa jamii, wataalamu na viongozi katika ngazi zote kila mmoja kutimiza wajibu wake katika harakati za kuudhibiti ugonjwa huu. Aidha, Mikoa yote nchini ni lazima ichukue hatua stahiki ikiwemo Mikoa ambayo haijapata mgonjwa na ile ambayo imepata ugonjwa na umedhibitiwa.

Tunawashukuru wadau wote wanaoshirikiana na Serikali, yakiwemo Mashirika ya Kimataifa kwa mchango wao mkubwa katika jitihada zetu za kupambana na Kipindupindu. Pamoja tukishirikiana tutaweza kuutokomeza ugonjwa huu.


No comments:

Post a Comment