Nchi yetu ina kingo za mito na
mabonde na maeneo mengi hatarishi ambamo watu wanaishi kinyume cha sheria, huku
wakiharibu mazingira na kuhatarisha maisha yao. Kutokana na uhaba wa
makazi, hali ni mbaya zaidi katika mabonde ya Jiji la Dar es Salaam, hasa bonde
la Mto Msimbazi.
Serikali za awamu zote, zimekuwa
zikifanya jitihada za kuwaondoa wakazi wa maeneo ya mabondeni wanaoishi katika
maeneo hayo kinyume cha sheria lakini mafanikio yamekuwa si ya kuridhisha.
Serikali ya Awamu ya Tano, ambayo
moja ya misingi yake mikuu ni utii wa sheria za nchi, imeanza jitihada za
kuwaondoa wakazi hawa.
Tuliamua kuanza na Bonde la Mto
Msimbazi kwasababu ndiko kwenye watu wengi na athari kubwa.Sababu zetu kuu za
kufanya zoezi hili ni kusafisha mabonde na mito katika jiji la Dar es Salaam na
mazingira yanayozunguka ni:-
Kunusuru
maisha ya wananchi wanaoishi katika mazingira
hatarishi. Eneo la Bonde la Mto Msimbazi lilitangazwa kuwa ni eneo hatarishi
kuishi binadamu tangu mwaka 1949 na baadaye 1979.
Kupanua
uwezo wa mito ya Dar es Salaam ili kupitisha
maji ya mvua kwa kasi kubwa, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea mafuriko na
maafa wakati wa mvua nyingi;Kuzuia milipuko ya magonjwa, hasa ya kipindupindu,
hasa wakati wa mvua;
Kuzuia
eneo hilo kuendelea kutumika kama maficho
ya wahalifu na uhalifu;
Kutoa
nafasi kwa Serikali kuandaa na kuendeleza
eneo hilo kwa mujibu wa sheria za nchi na mipango miji;
Utaratibu
wa Zoezi
Kabla ya nyumba kubomolewa, taasisi
hizi zinashirikiana kuhakiki iwapo nyumba anayokaa mkazi ina nyaraka za umiliki
na vibali vya ujenzi na iwapo nyaraka hizo zina uhalali wowote.
Nyumba ambazo zimethibitika kuwepo
katika maeneo yasiyostahili ndio zinawekwa alama X kuashiria kwamba wakazi
wanapaswa kuhama au kubomoa. Baada ya hapo, mkazi hupewa muda wa kubomoa na
kuhama mwenyewe.
Kutokana na utaratibu huu, sehemu
kubwa ya nyumba zinazobomolewa ni zile ambazo watu wamekwishaamua kubomoa
wenyewe.
Baada ya hapo, alama huwekwa
kuonyesha mpaka wa bonde. Katika zoezi hili, imebainika kwamba sehemu kubwa ya
wakazi wa maeneo ya mabondeni ni wapangaji huku wamiliki wakikaa sehemu
nyingine salama.
Serikali pia imeweka Dawati la
Malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Tathmini
ya Zoezi
Jana, terehe 7 Januari 2016,
Mawaziri watatu (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, TAMISEMI; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais; pamoja na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii), walifanya mkutano wa kutathmini
zoezi la kuhamisha wakazi wa mabondeni katika Jiji la Dar es Salaam.
Mkutano huo ulipokea ripoti ya timu
ya wataalam wa Wizara mbalimbali, inayoongozwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na
Usimamizi wa Mazingira, ambayo, pamoja na mambo mengine ilibainisha kwamba
sehemu kubwa ya kubaini makazi yaliyojengwa kinyume cha Sheria katika Bonde la
Mto Msimbazi imekamilika.
Ripoti ilieleza kwamba, hadi sasa,
wananchi katika nyumba 774 wamehama na nyumba hizo kubomolewa. Ilielezwa
pia kwamba kabla ya mkazi kuombwa kuhama, uhakiki kuhusu uhalali wa
makazi anayoishi hufanywa.
Kutokana na uhakiki huo, jumla ya
wakazi 20 walikuwa na hati halali za makazi na wakazi 119 walikuwa na leseni za
makazi za muda mfupi.
Hawa watu hawakuhamishwa. Mawaziri
walipokea maelezo kuhusu changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika zoezi
hilo.
Baada ya
tafakuri na mjadala, Mawaziri hao walitoka na msimamo ufuatao, kama uamuzi wa
Serikali: -
1.Zoezi la kuwaondoa wananchi
waishio katika bonde la Mto Msimbazi (eneo hatarishi) litaendelea kwa utaratibu
ambao hautaleta mateso na usumbufu kwa wananchi;
2.Katika awamu hii, zoezi litajikita
katika Bonde la Mto Msimbazi tu.
3.Kwa wakati huu, watakaohitajika
kuhama ni wale tu ambao makazi yao yamo NDANI kabisa ya bonde, kwenye miteremko
ya kuingia bondeni na kwenye KINGO za mto;
4.Wale watakaokuwa na nyaraka halali
walizopewa na mamlaka za umma, zilizowamilikisha na kuwaruhusu kujenga katika
bonde hilo, hawatahamishwa bila kupewa sehemu nyingine za kujenga. Na watumishi
wa umma waliowamilikisha maeneo hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu na
kisheria;
5.Serikali, ndani ya siku tatu
zijazo, itaanza zoezi la kuzoa kifusi na kusafisha maeneo ambapo ubomoaji
umefanyika.
6.Serikali itaheshimu amri za
mahakama kuhusu mapingamizi yaliyowekwa na baadhi ya wakazi wa mabondeni lakini
pia itafuatilia kesi hizi ziishe haraka ili taratibu zinazofuatia zifanyike;
7.Serikali itawachukulia hatua za
kinidhamu watumishi wake wanaoendesha zoezi hili kinyume na misingi ya sheria
zinazotekelezwa, na kinyume na misingi ya haki na uwazi, ikiwemo wanaoweka
alama za X zaidi ya mita zilizowekwa kisheria. Limeanzishwa dawati la
malalamiko katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya
kupokea malalamiko au maswali kuhusu zoezi hili.
8.Nyumba na majengo ya miaka mingi,
yaliyokuwepo miaka mingi kabla ya kutungwa kwa Sheria zinazotekelezwa kwa zoezi
hili, hayatabomolewa isipokuwa tu pale maisha ya wakazi yapo hatarini.
Wanaoishi katika makazi hayo watapewa miongozo ya hatua za kuhifadhi mazingira
na kujiokoa na maafa;
9.Serikali haina dhamira ya kubomoa
mahoteli makubwa ya siku nyingi yaliyo karibu na fukwe katika maeneo ya Masaki.
Wamiliki wa mahoteli haya watapewa masharti na miongozo ya kuhifadhi mazingira
kwa mujibu wa Sheria.
10.Serikali inaweka uratibu wa
karibu zaidi miongoni mwa taasisi zake ili hatua za utekelezaji wa sheria za
nchi zisiwe chanzo cha taharuki katika jamii.
11.Serikali haina dhamira ya
kuwatesa wananchi wake kwa kuwalazimisha kuhama katika makazi yao bila sababu
za msingi. Lakini pia Serikali haiwezi kuruhusu wananchi waendelee kukaa katika
maeneo ambayo ikinyesha mvua kubwa maisha yao yapo hatarini.
Itakumbukwa kwamba katika
mafuriko ya mwaka 2011, wananchi 49 waishio mabondeni walipoteza maisha. Kwa
mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Hali ya Hewa, mwaka huu zinatarajiwa kunyesha
mvua kubwa kuliko zilizowahi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.
12. Serikali inafuatilia kwa
karibu kwa mamlaka za Serikali za Mitaa juu ya taarifa za wananchi wanaohitaji
msaada maalum wa kibinadamu.
Suala la
Mchungaji Getrude Rwakatare
Mkutano ulipokea taarifa kuhusu
suala linaloongelewa sana la nyumba ya Mchungaji Rwakatare. Ilielezwa
kwamba Mchungaji Rwakatare amejenga nyumba yake pahali ambapo amezuia mtiririko
wa mto kwa kujaza kifusi ili kupata eneo zaidi katika eneo la miti ya mikoko,
kinyume kabisa na Sheria tatu muhimu.
Pia ilielezwa kwamba tangu wakati
ujenzi unaanza jitihada za kumsimamisha zilifanyika na mamlaka za Serikali za
Mitaa lakini ikashindikana kutokana na sababu mbalimbali. Pale Baraza la Taifa
la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira lilipoingilia kati na kutaka kuibomoa
nyumba hiyo, Baraza lilishtakiwa mahakamani.
Wakati kesi inataka kuanza
kusikilizwa, mwanasheria mdogo wa Baraza, yeye mwenyewe bila kuagizwa wala
kuwaarifu wakubwa zake, mnamo tarehe 11 Mei 2015, aliingia makubaliano na
mawakili wa Mchungaji Rwakatare kwa niaba ya Baraza ya kuondoa kesi hiyo
mahakamani na kukubali, kwa niaba ya Baraza, kutombughudhi kabisa Mchungaji Rwakatare.
Makubaliano hayo yalisajiliwa na
Mahakama kama hukumu tarehe 13 Mei 2015. Mwanasheria huyo alificha makubaliano
hayo kwa miezi mitano hadi Oktoba 2015, yalipogundulika na mtumishi mwingine wa
Baraza. Mkutano ulielezwa kwamba Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, kwa
kufuata taratibu zote, alishaagiza kufukuzwa kazi, kukamatwa na kufunguliwa
mashtaka kwa mwanasheria huyo.
Mwanasheria huyo alifukuzwa kazi
siku ya juzi tarehe 6 Januari 2016 na taarifa zake zimekwishafikishwa
TAKUKURU.
Vilevile, Ofisi ya Makamu wa Rais,
iliiagiza Baraza kufungua shauri mahakamani la kuomba “makubaliano” kati yake
na Mchungaji Rwakatare yawekwe pembeni kwasababu yalipatikana na njia ya
udanganyifu. Shauri hilo lilifunguliwa tarehe 29 Disemba 2015.
Kuhusu
Karakana ya Mradi wa Mabasi Yaendayo kwa Kasi (DART)
Mkutano pia ulijulishwa kuhusu hoja
inayozungumzwa kwamba wananchi wanaondolewa katika maeneo ya kuishi mabondeni
lakini mradi wa DART umeachwa.
Mkutano ulielezwa kwamba
Sheria ya Mazingira (kifungu 57 (2)) inatoa nafasi ya kutolewa ruhusa kwa
miradi/shughuli zenye maslahi ya taifa kufanyika katika maeneo ya mabondeni, na
kwamba Waziri mwenye dhamana ya mazingira anaruhusiwa kutoa miongozo ya namna
ya shughuli hizo zinavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira.
Mradi wa DART ulipata kibali
hicho na una mkataba na Baraza la Mazingira kuhusu hatua za hifadhi ya
mazingira zinazopaswa kutekelezwa katika mradi huo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA MAKAMU WA RAIS
08.01.2016
No comments:
Post a Comment