Friday, June 03, 2016

AFRIKA YATAKIWA KUIMARISHA UTAWALA WA SHERIA: BALOZI MAHIGA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mashariki Balozi Augustine Maiga akitoa maelezo kwa wadau waliohudhuria mkutano wa Utawala wa Sheria na Utawala Bora (hawapo pichani) uliofanyika jijini Dar es salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Maiga akiongea jambo na Balozi wa Italia Nchini Mhe. Luigi Scotto baada ya kumaliza mkutano wa Utawala wa Sheria na Utawala Bora uliofanyika  jijini Dar es salaam.
Wadau wa Mkutano wa Utawala wa Sheria kutoka nchi mbalimbali duniani wakifatilia kwa makini mkutano wa Utawala wa Sheria na Utawala Bora ili kufikia agenda ya mwaka 2030 na 2063 ya malengo ya millennia uliofanyika leo jijini Dar es salaam.Picha na Ally Daud- Maelezo

Na: Immaculate Makilika- MAELEZO, 
Dar es Salaam

BARA la Afrika limetakiwa kuimarisha Utawala wa Sheria kupitia vyombo vya dola ikiwemo mahakama na polisi ili kuisaidia mfumo huo kutetea maslahi ya wanyonge.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga wakati alipokuwa akifunga Mkutano wa siku mbili wa Kimataifa kuhusu Utawala wa Sheria na Utawala bora.

“Lazima Afrika iimarishe vyombo vyake vinavyosimamia Utawala wa sheria na Utawala bora kama Polisi na Mahakama pamoja na kuwa na msimamo wa Bara katika kuzungumzia masuala mbalimbali” alisema Balozi Mahiga Balozi Maiga alisisitiza kuwa rushwa imekua adui mkubwa katika Utawala wa Sheria, hivyo ni lazima suala hilo lipatiwe ufumbuzi ili haki iweze kutendeka kwa watu wote.

Aidha, Balozi Maiga amemshukuru Balozi wa Italia nchini Mhe. Luigi Scott kwa kufanikisha mkutano huo pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Sheria (IDLO) Bibi. Irene Khani kwa uamuzi wa wake wa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

“Mkutano huu ni wa kihistoria utasaidia kuleta mageuzi katika Taasisi ama Vyombo vinavyosimamia masuala ya Sera na Sheria ambayo yatachochea maendeleo mazuri katika nchi za Afrika” alisema Balozi Mahiga.

Mkutano huo unaomalizika leo ulikua na kauli mbiu isemayo “Kufikia agenda ya 2030 na agenda ya 2063: Utawala wa Sheria kwa Maendeleo Endelevu ya Afrika”, umehusisha wadau mbalimbali wakiwemo Mawaziri, kutoka nchi mbalimbali za Afrika, Mabalozi kutoka ndani na nje ya Afrika pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya kutetea Haki za Binadamu ulimwenguni.

No comments:

Post a Comment