Wednesday, May 18, 2016

WADAU WA MAZINGIRA WAANDAA TAMASHA LA MAZINGIRA LITAKALOMHUSISHA RAIS MSTAAFU DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE NA RAIS DKT. JOHN POMBE MAGUFULI.

Rais mstaafu wa awamu ya nne Daktari Jakaya Mrisho Kikwete.
Na. Lilian Lundo – Maelezo.
Watanzania  wameombwa kutoa  maoni kuhusu njia zipi  zitumike kutunza mazingira na kukomesha uvuvi haramu wilayani  Temeke katika tamasha  la mazingira litakalofanyika Mei 27, 2016 kwenye fukwe za Sunrise – Kigamboni.

Akizungumza na waandishi wa habari  katika mkutano uliofanyika  jijini Dar es Salaam, Katibu wa CFMA (Collaborative Fisheries Management Area) Godfrey  Maduhu alisema  wao wakiwa wadau wa mazingira wameandaa tamasha lenye lengo la kupiga vita uvuvi  haramu na utunzaji wa mazingira.

Maduhu alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano huo, ambao ulishirikisha Mtandao  wa Usimamizi Shirikishi wa Kusimamia Rasimali za Pwani na Bahari,  Balozi wa kujitolea na wadau sekta ya mazingira(WWF).

“Tunapenda kuujulisha umma kuhusiana na tamasha litakalohusisha wadau mbalimbali wa mazingira, litakalokwenda kwa jina la ‘kwa heri Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, karibu Dkt. John Pombe Magufuli,’ lenye lengo la kupiga vita masuala ya uvuvi haramu na kuhamasisha jamii juu ya usimamizi na utunzaji wa mazingira,” alisema Maduhu.

Aidha, Maduhu alisema kwamba lengo la tamasha hilo ni kupanga mikakati juu ya  utunzaji na uendelezwaji mzuri wa mazingira na kusikia kauli kutoka viongozi ngazi ya juu hususani kuhusiana na changamoto katika suala la utunzaji wa mazingira.

Maduhu alisema kwamba kama hakutakuwepo na mikakati ya kushughulikia  changamoto juu ya uvuvi haramu, Serikali itapoteza mapato mengi kwa kupoteza wateja kutokana na milipuko ya mara kwa mara  katika fukwe za bahari  na kupelekea watalii  kuhofia maisha yao.

 Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kupungua kwa kipato cha wananchi na Taifa kutokana na kupungua kwa samaki  katika Bahari ya Hindi na ongezeko la wagonjwa wa kansa kutokana na kula samaki waliouliwa kwa kutumia baruti.

Kwa upande wake, Balozi wa mazingira wa kujitolea  Omary Kombe alisema kuwa, mazingira bado machafu hivyo ameitaka Serikali kuendelea kukazia suala la usafi ikiwezekana hata kwa kuweka faini kwa mtu atakayeonekana kuchafua mazingira.

Tamasha hilo litahusisha viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya Serikali za Mtaa, Wilaya, Mkoa na Taifa.Pia kutakuwa na ukusanyaji wa maoni  kutoka kwa  wananchi juu ya njia gani zitumike kuboresha utunzaji mazingira na kukomesha  uvuvi haramu.

No comments:

Post a Comment