Mtaalam Mshauri wa Master Card Foundation Gabriel Kivuti akieleza jambo kwa waandishi wa habari juu ya kushiriki shindano la kuongeza kipato lijulikanalo kama “Scaling Competition” kwa makundi yanayoruhusiwa kushiriki shindano hilo kuwa ni pamoja na vikundi vya akiba, bima ndogo ndogo na mifumo ya umoja wa fedha, fomu za maombi na mwongozo wa kushiriki shindano hilo zinapatikana katika tovuti ya www.frp.org .
Na: Lilian Lundo - Maelezo
Watanzania wameombwa kujitokeza kwa wingi kushiriki shindano la kuongeza kipato lijulikanalo kama “Scaling Competition” kwa kutuma maombi yao shirika la “Master Card Foundation, Fund For Rural Prosperity” ili kupanua na kuimarisha upatikanaji wa fedha Vijijini Tanzania.
Hayo yalisemwa na Mtaalam Mshauri wa Master Card Foundation Gabriel Kivuti leo, jijini Dar es Salaam katika semina ya namna shirika hilo linavyofanya kazi na jinsi ya kushiriki shindano la mwaka 2016 ili kupata washindi watakaopata msaada wa kifedha na kuboresha ushirikishwaji wa kifedha kwa wakulima wadogo Afrika.
“Master Card Foundation inafanya kazi na mashirika yenye maono ili kuleta zaidi upatikanaji wa elimu, mafunzo ya ujuzi na huduma za kifedha kwa watu wanaoishi katika umaskini barani Afrika, ikiongozwa na dira ya kuboresha mafunzo na kuongeza ushirikishwaji wa upatikanaji wa kifedha ili kupunguza umaskini,” alisema Kivuti.
Kivuti alisema kuwa, kaya nyingi za vijijini barani Afrika hazishirikishwi katika masuala ya kifedha na zaidi ya asilimia 70 za familia Kusini mwa Jangwa la Sahara sehemu kubwa ya mapato yao yanatokana na shughuli za kilimo, wakati huohuo watoa huduma za kifedha wanakabiliana na changamoto kadhaa katika kuifikia jamii, hivyo Master Card likaamua kusaidia miradi ambayo ina uwezo wa kuleta mabadiliko chanya.
Aidha, Kivuti alitaja makundi yanayoruhusiwa kushiriki shindano hilo kuwa ni pamoja na vikundi vya akiba, bima ndogo ndogo na mifumo ya umoja wa fedha, fomu za maombi na mwongozo wa kushiriki shindano hilo zinapatikana katika tovuti ya www.frp.org .
Jumla ya dola za Kimarekani milioni 10.6 zimetolewa kwa washindi wa mwaka 2015 kwa ajili ya maendeleo Vijijini, kampuni zilizoshinda ni APA Insurance Ltd kutoka Kenya, Finserve Afrika Ltd/Equitel kutoka Uganda, M-KOPA LLC kutoka Tanzania, Musoni Kenya Ltd kutoka Kenya na Olam Uganda Ltd kutoka Uganda. Kupitia kampuni hizo takribani watu milioni nane wanaoishi maeneo ya Vijijini watakuwa na fursa ya kupata huduma za kifedha ifikapo mwaka 2020.
No comments:
Post a Comment