Tuesday, May 10, 2016

WANANCHI WASHAURIWA KUTUMIA HUDUMA ZA MSAADA WA KISHERIA.

Na Beatrice Lyimo- MAELEZO

DAR ES SALAAM.
Serikali imewataka wananchi wasio na uwezo wa kuweka Mawakili au kulipa huduma za kisheria kutumia Mpango wa Huduma za Msaada wa Kisheria kupitia Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria na Mashirika yaliyosajiliwa kwa ajili hiyo.

Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka  Wizaraya Katiba na Sheria  Bi. Sheiba Bulu alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu huduma hiyo inayotolewa na Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria na Mashirika yaliyosajiliwa kwa ajili hiyo.

Amesema kuwa lengo kuu la huduma hiyo ni kuhahikisha kila mwananchi anapata haki katika mamlaka husika za utoaji haki na kwa wakati.

“Sekretarieti ya Msaada wa Kisheria inatoa huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi ambao ni wahitaji wa msaada wa huduma za kisheria na kuwapa ushauri juu ya masuala mbalimbali yanayowakabili,” aliongeza Bi. Sheiba.

Aidha, kwa upande wake Wakili wa Serikali Mkuu kutoka Wizara hiyo, Charles Mmbando amezitaka asasi na mashirika yanayojishughulisha na huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi kujitangaza  ili kuzidi kutambulika katika jamii  kwani wizara  yake inatambua na kuthamini mchango unaotolewa na mashirika hayo.

Mpango huo ulianzishwa mwaka 2012 ili kuwezesha asasi na Mashirika yasiyokuwa ya kiserikali kupanua wigo wa huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi waishio kwenye maeneo ambayo hawawezi kulipia gharama za mawakili nchini.

No comments:

Post a Comment