Friday, May 27, 2016

KIBITI KUFANYA KONGAMANO LA KUIPOKEA WILAYA MPYA KWA KUSHIRIKI SHUGHULI MBALIMBALI ZA MAENDELEO.

Na Daudi Manongi-MAELEZO

Viongozi wa umoja na wadau wa maendeleo wilaya mpya ya kibiti (UWAWAMAKI) mkoani Pwani umepanga kufanya kongamano la kuunga mkono tamko la Serikali ya awamu ya Tano ya Mhe.John Pombe Magufuli kwa kuifanya Kibiti kuwa Miongoni mwa Wilaya mpya siku ya jumapili tarehe 29 saa nne asubuhi kwenye ukumbi wa Shule ya Sekondari TEDEO Temeke jijini Dar es Salaam.
Akiongea na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Katibu wa umoja huo Bw.Selemani Ndumbogani  amesema kuwa wanakibiti wamefarijika sana na kauli ya Serikali ya Kuipatia Kibiti wilaya jambo ambalo lilikuwa kilio cha muda mrefu ikiwa ni takribani zaidi ya miaka arobaini tangu uhuru na kuongezea kuwa walikuwa mbali sana na huduma muhimu za Serikali.

Pia umoja huo umeomba wana jimbo la kibiti hususani Rufiji kujitokeza kwa wingi kwenye kongamano hilo ili liwe lenye mafanikio makubwa.
Miongoni mwa mambo yaliyoandaliwa kufanywa ni pamoja na usafishaji wa mitaa,soko, maeneo ya standi ,eneo litakalojengwa wilaya,na kuendesha dua kwa madhehebu mbalimbali ya dini ili kuiombea kheri wilaya ya kibiti,Pia kuiombea nchi na Rais wetu wa Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe.John Pombe Magufuli na Mhe.Kassim Majaliwa kuishi kwa amani na usalama katika kusimamia shughuli za Taifa.
Mwaka huu mwezi Februari Rais wa awamu ya tano Dr.John Pombe magufuli alitangaza kuipandisha adhi wilaya hiyo mpya ya kibiti ambapo kwa mujibu wa katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imempa mamlaka rais ya kugawa nchi kwa kadri ambavyo atakavyoona inafaa.


No comments:

Post a Comment