Anitha Jonas –
MAELEZO
Tarehe 23/05/2016
Dar es Salaam.
SERIKALI imesema kuwa
mtu yeyote atakayekamatwa kwa kosa la husisha au kushawishi mtoto kujiingiza
katika matumizi au biashara ya dawa za kulevya atahukumiwa kifungo cha miaka
isiyopungua 30.
Hayo yamesema na Mkuu
wa Kitengo cha Elimu, Habari na Takwimu wa Tume ya kuratibu na kudhibiti wa
Dawa za Kulevya, Amani Msami kupitia Taarifa ya tume hiyo kwa vyombo vya
habari.
Msami alisema adhabu
hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya kudhibiti na kupambana na Dawa za Kulevya Na.5
ya mwaka 2015 tofauti na Sheria ya Kuzuian Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya
Na. 9 ya mwaka 1995 iliyokuwa na mapungufu.
Alisema mbali na
adhabu hiyo, sheria hiyo mpya imeweka adhabu ya kifungo cha maisha na faini ya
shilingi Milioni 200 kwa kumiliki mitambo ya kutengeneza dawa za kulevya.
Msami aliongeza kuwa
Sheria hiyo pia imeweka adhabu kali ya kifungo cha maisha pamoja na faini
isiyopungua Shilingi Bilioni moja kwa watu wanaofadhili biashara ya Dawa za
Kulevya.
“Aidha, sheria hii
imeweka adhabu kali ya kifungo cha maisha pamoja na faini isiyopungua Shilingi
Bilioni moja kwa watu wanaofadhili biashara ya Dawa za Kulevya ambao mara
nyingi ni watu wenye uwezo,”alisema Msami.
Mkuu huyo wa Kitengo,
alisema Serikali kupitia vyombo vya Dola iliwabaini, kuwakamata na kuwachukulia
hatua za kisheria baadhi ya wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa dawa za
kulevya.
Aliwataja baadhi ya
watuhumiwa wakubwa wa dawa hizo waliokamatwa na kuchukuliwa hatua kuwa ni Ali Khatibu haji (maarufu kwa jina la Shkuba,
Mohammed Mwarami (maarufu kwa jina la Chonji na Mwanaidi Mfundo (maarufu kwa
jina la Mama Leila).
Msami alisisitiza
wito wa Serikali kwa wananchi kutoa ushirikiano wa dhati kwa ajili ya kutoa taarifa
kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa ya kulevya ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
No comments:
Post a Comment