Wednesday, May 18, 2016

WANAJESHI WA DRC WANAWAUA RAIA MASHARIKI MWA NCHI HIYO

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa katika kamati ya vikwazo vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wametoa ripoti na kusema maafisa wa kijeshi nchini humo wanahusika na mauaji ya raia.

Ripoti hiyo inasema kuwa baadhi ya wanajeshi wa DRC kwa uungaji mkono waasi kutoka Uganda walioko mashariki mwa DRC wanahusika katika kuwaua kinyama raia wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa nyaraka za Umoja wa Mataifa, Muhindo Mundos, mmoja kati ya makamanda wa ngazi za juu wa jeshi la DRC amekuwa akiwaunga mkono kifedha na kijeshi waaasi wa ADF kutoka Uganda ambao wanahusika na mauaji ya raia wa jimbo la Kivu Kaskazini.
Weledi wa mambo wanaamini kuwa, uungaji mkono wa baadhi ya wanajeshi wa DRC kwa waasi wa Uganda ndicho chanzo kikuu cha machafuko mashariki mwa DRC na kuwa jambo hilo linahesabiwa kuwa ni uhaini wa wazi kwa maslahi ya taifa na watu wa Kongo.
Rais Joseph Kabila wa DRC amekuwa akisisitiza kuhusu umuhimu wa kushirikiana jeshi la DRC na majeshi ya Sudan Kusini na Uganda katika kung'oa mizizi ya makundi ya waasi katika eneo hilo. Lakini oparesheni za pamoja za majeshi ya nchi hizo bado hazijazaa matunda katika kuwaangamiza kikamilifu waaasi.
Kufichuliwa kuhusika maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la DRC katika mauaji ya raia ni jambo ambalo linaweza kuwa moja ya sababu za kushindwa jitihada za kumaliza machafuko mashariki mwa nchi hiyo.
Wakati huo huo, baada ya kukimbia askari wa DRC kutoka katika eneo la Bashali Mokoto na Masisi katika Jimbo la Kivu Kaskazini, waasi wenye asili ya Rwanda sasa wameyakalia kwa mabavu maeneo hayo.
Haya yanajiri katika hali ambayo tokea tarehe 22 Machi jeshi la DRC lilianzisha oparesheni maalumu ya kuwatimua waasi hao kutoka Rwanda sambamba na kurejesha utawala wa sheria na usalama katika eneo hilo.
Inaelekea kuwa, waasi kutoka Rwanda na Uganda wanalenga kuchukua udhibiti wa migodi iliyojaa almasi katika maeneo ya mashariki mwa DRC. Waasi hao hivi sasa hawana wasiwasi wala hawaogopi wanapotekeleza jinai za kuwaua raia na kupora mali zao. Hivi sasa maelfu ya wakaazi wa eneo hilo wameanza kukimbilia nchi jirani wakihofia hujuma za waasi.
DRC inapakana na nchi 9 na hivyo iwapo serikali ya nchi hiyo haitaweza kuwazuia wanajeshi kuwasaidia waasi katika kuwaua raia, basi yamkini hali ikazidi kuwa mbaya katika eneo la Maziwa Makuu. Vita vya ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo vilimalizika mwaka 2003. Kutokana na vita hivyo kuhusisha nchi takribani 8 za Kiafrika, vita hivyo vilitajwa kuwa ni 'Vita vya Dunia vya Afrika.
Rwanda na Uganda ni waitifaki wa karibu wa Marekani katika eneo la Mashariki na katikati mwa Afrika, na zilianzisha vita dhidi ya serikali ya wakati huo ya DRC kwa sababu ilikataa kutekeleza matakwa yao haramu.
Hivi sasa ushirikiano wa baadhi ya maafisa wa jeshi la DRC na waasi wa Uganda katika kuwaua raia mashariki mwa nchi hiyo yamkini zikawa cheche za kuzuka tena vita baina ya DRC, Uganda na Rwanda.

No comments:

Post a Comment