Tuesday, May 10, 2016

MEGAWATI 100 KUTOKANA NA JOTOARDHI KUZALISHWA MIAKA 7 IJAYO:

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo (pichani) akisoma hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa siku tatu jijini Dar es Salaam uliokutanisha wataalam kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujadili taarifa ya mtaalam mwelekezi kuhusu utafiti uliofanywa katika Ziwa Ngozi lililopo mkoani Mbeya ambapo kuna viashiria vya jotoardhi pamoja na eneo la Kibiro nchini Uganda.
Wataalam mbalimbali wakifuatilia kwa makini hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo ( anayeonekana mbele kwa mbali)
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo (wa nne kutoka kushoto waliokaa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo mara baada ya ufunguzi.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Imeelezwa kuwa Tanzania inatarajia kuzalisha megawati 100 ndani ya kipindi cha miaka saba ijayo na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya nishati, Dk. Juliana Pallangyo katika mkutano uliokutanisha wataalam kutoka nchi mbalimbali kwa ajili ya kujadili taarifa ya mtaalam mwelekezi kuhusu utafiti uliofanywa katika Ziwa Ngozi lililopo mkoani Mbeya ambapo kuna viashiria vya jotoardhi pamoja na eneo la Kibiro nchini Uganda.

Wataalam katika mkutano huo ulioandaliwa na Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania (TGDC) kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje Iceland, wanatoka katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Marekani, New Zealand na Djibouti.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo wa siku tatu Dk. Pallangyo alisema kuwa kutokana na ugunduzi wa nishati ya jotoardhi nchini Tanzania, serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ndani ya kipindi cha miaka saba ijayo inazalisha megawati 100 zitakazoongezwa kwenye gridi ya taifa na hivyo kupunguza tatizo la upungufu wa umeme nchini.

Alisema kuwa serikali imeweka mkakati wa kuhakikisha kuwa nishati ya umeme inachangia katika ukuaji wa uchumi na kupelekea nchi kutoka kwenye orodha ya nchi masikini duniani na kuingia katika nchi zenye kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, kama Dira ya Maendeleo ya Taifa inavyofafanua.Aliongeza kuwa kuwepo kwa nishati ya uhakika kutavutia uwekezaji kwenye viwanda na kuzalisha ajira na nchi kupiga hatua kimaendeleo.

Alisisitiza kuwa Tanzania ina nishati ya kutosha ya jotoardhi yenye uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 5000 ambayo haijatumika bado ambapo serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi Tanzania ambayo ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Aliendelea kusema kuwa TGDC ilianzishwa Desemba 2013 kwa madhumuni ya kusimamia maendeleo ya jotoardhi nchini Tanzania na kuanza rasmi shughuli zake Julai 2014 jukumu lake kuu likiwa ni kutafiti, kuchimba na kutumia rasilimali za jotoardhi kwa uzalishaji umeme na matumizi mengine ya moja kwa moja.

No comments:

Post a Comment