Friday, May 27, 2016

CHUMBA CHA DEREVA TAX KUWA GUMZO KWA WAKAAZI WA MBEZI.

Na Ripota wa Sufianimafoto ,Dar
UKIHADITHIWA na kuonyeshwa chumba cha Dereva Tax anayeonekana kitaani na katika kazi zake akiwa amepiga pamba wala hutaamini masikio yako wala macho yako pindi utakapopata bahati ya kufika na kushuhudia chumba hicho kilichopo maeneo ya Gold Star Mtaa wa Mbezi Mtoni Bondeni jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wa habari hii alipata fursa ya kufika na kushuhudia yale yaliyokuwa yakisemwa na baadhi ya wakazi wa mtaa huo jana majira ya saa tano usiku baada ya kutokea mtafaruku na sintofahamu katika nyumba hiyo ya Mama Mwakajinga, anayoishi Dereva huyo aliyejulikana kwa jina la Steven al-maarufu kama ‘NYATI’.

Akizungumza na mwandishi kuhusu tukio hilo, Mama mwenye nyumba, alisema kuwa siku ya Mei 23, akiwa ameketi uwaji karibu kabisa na Chumba cha Jamaa huyo huku akichambua mboga, alihisi harufu kali na mbaya iliyokuwa ikivuma kutoka chumbani kwa Dereva huyo aliyepanga katika nyumba yake tangu mwaka 2008 na kuona wadudu aina ya funza wakitoka chumba hicho kupitia chini ya mlango.

Kesho yake Mei 24 baada ya kuona wadudu hao huku harufu ikizidi kuwa kali, alimuita jirani yake na kumshirikisha jambo hilo huku wote wakishikwa na butwaa na kuwa na mashaka na chumba hicho.

Mei 25 Mama mwenye nyumba aliamua kwenda kwa Mjumbe wa eneo hilo Badili Makoye, kutoa taarifa juu ya wasiwasi uliotanda katika nyumba hiyo na kuongozana na Viongozi wengine, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Frank Kyaruzi, Wajumbe wengine  Abdalla Mlaliya na Matrida Paston, waliofika na kujionea hali halisi ya chumba hicho.

Baada ya viongozi hao kufika eneo la tukio walimuamuru Mama mwenye nyumba kwenda kutoa taarifa kituo cha Polisi.  Mama huyo alitekeleza agizo na kwenda kuripoti Kituo cha Mbezi Garden na kuongozana na Mkuu wa Kituo hicho na baadhi ya askari hadi nyumbani na kukuta hali hiyo ya sintofahamu.

Walipofika eneo la tukio na kushuhudia hali hiyo, Mkuu wa Kituo aliamuru mlango huo uvunjwe huku wananchi na Viongozi wa Mtaa huo wakishuhudia na kuingia ndani ambako walikuta Chumba kizima kikiwa kimejaa Chupa za Plastiki zilizojaa mikojo, Mifuko ya Rambo ikiwa na Vinyesi, Feni moja iliyochomekwa kwenye Soketi ya Umeme ukutani, Pakiti nyingi tupu za Sigara aina ya Embassy na Kondomu zilizotumika na zisizotumika.

Baada ya zoezi hilo, Mwenyenyumba alimpigia simu mpangaji wake na kumtaka kurejea nyumbani, lakini Dereva huyo alijibu kuwa kwa muda huo alikuwa mbali maeneo ya Kunduchi na kuahidi kuwagongea usiku pindi atakaporejea.

Hadi Mwandishi anaondoka eneo la tukio majira ya saa tano usiku bado wakazi wa maeneo hayo walikuwa wamejazana nje ya Chumba hicho wakiendelea kumsubiri arudi ili kupata ukweli kuhusu mambo waliyoyaona katika chumba chake.

Aidha Mama mwenye nyumba alisema kuwa mpangaji wake huyo, tangu alipohamia katika nyumba hiyo mwaka 2008, hakuwahi kumuona akiingia na mwanamke katika chumba hicho, wala kumuona mgeni wa aina yeyote kwa Dereva huyo,jambo lililomshangaza kukuta Kondom zilizotumika katika chumba hicho. Ama kweli ukistaajabu ya Mussa utayaona ya Filaun.

Leo hii Mei 27, Mama mwenye nyumba ameripoti kuwa mpangaji wake huyo,hajatokea nyumbani hapo tangu kutokea kwa tukio hilo ambapo leo, amechukua uamuzi wakuwalipa vijana wa mtaa huo ili wasafishe chumba hicho.

"Tayari tumewalipa pesa vijana kiasi cha sh.200,000/= ili wafanya usafi na wameshamaliza na kwenda kufukia bonde la mto Mbezi." Amesema mama huyo
Wananchi na mwenye nyumba wakifungua mlango 
Chupa zinazodaiwa kuwa na mikojo zikiwa zimetapakaa ndani ya chumba hicho.
Source Mpekuzi,

No comments:

Post a Comment