Friday, May 27, 2016

SERIKALI YAPIGA MARUFUKU USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI WA HIFADHI ZA TAIFA NJE YA NCHI KWA MIAKA 3.

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne akijibu hoja na michango mbalimbali ya wabunge zilizoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 135.7.
Baadhi ya wabunge wakimpongeza wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe mara baada ya Bajeti ya Wizara hiyo kupitishwa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 135.7.
Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akimweleza jambo Mbunge wa Bunda mjini Mhe. Esther Matiku (CHADEMA) nje ya ukumbi wa Bunge mara baada ya kupitishwa kwa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017.

Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii bungeni mjini Dodoma. 


Serikali imesimamisha utoaji wa vibali na uuzaji wa wanyama hai kutoka katika hifadhi za Taifa kwenda nje ya Tanzania kwa kipindi cha miaka 3 mpaka hapo itakapotangazwa tena.Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe ametoa agizo hilo bungeni mjini Dodoma wakati akijibu hoja na michango mbalimbali ya wabunge iliyoelekezwa kwenye wizara hiyo wakati wa Majumuisho ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2016/2017 ambayo imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 135.7.

Prof. Maghembe ameiagiza Idara ya Wanyamapori ipange na kuweka utaratibu mpya utakaotumika kusimamia biashara hiyo pindi itakaporejeshwa tena baada ya kumalizika kwa muda wa zuio la Serikali la miaka 3 ikizingatia mazingira ya uhifadhi wa wanyama hao.

USAFIRISHAJI WA WANYAMA HAI  NJE YA NCHI.

Amesema kumekuwa na taarifa za baadhi ya watanzania wasio waaminifu ambao wamekua wakijihusisha na vitendo vya kusafirisha wanyama hai waliokatazwa kinyume cha utaratibu jambo ambalo limeisababishia Serikali ipoteze mapato kutokana na wanyama hao.

Akielezea kuhusu wanyama wanaoruhusiwa kusafirishwa nje ya nchi kama nyani, Kenge,ndege, kobe, wadudu na tumbili amesema wanyama hao wamekuwa wakisafirishwa kinyume na utaratibu na baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwa ajili ya kutumiwa na makampuni ya kimataifa kwenye shughuli za utafiti wa kisayansi wa tiba na chanjo.

Amesema makampuni hayo yamekuwa yakinufaika binafsi kwa kupata fedha nyingi pindi yanapofanikiwa kupata chanjo au tiba husika huku maeneo waliokotoka yakipata fedha kidogo jambo ambalo serikali ya awamu ya tano imeamua kulifanyia kazi.

UTALII KUSINI MWA TANZANIA NA MAENEO MENGINE. 

Amesema Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya uboreshaji wa Utalii wa Kusini ili kuweka mazingira wezeshi na kuondoa vikwazo vilivyokuwa vikisababisha watalii kushindwa kufika katika maeneo ya hifadhi za Taifa eneo la ukanda wa kusini mwa Tanzania.

Baadhi ya maeneo yatakayoshughulikiwa ni gharama ya usafiri wa ndege kwenda na kurudi katika maeneo hayo kuwa kubwa hadi kufikia Dola za kimarekani 1800 jambo ambalo limekuwa kikwazo kwa watalii hao.

Amesema Serikali itaanzisha vituo vya kuwekea mafuta ya ndege mahali vilipo vivutio vya utalii ili kuziwezesha ndege ndogo kufika kwa urahisi na kupata huduma ya kuongeza mafuta hivyo kupunguza gharama kwa wasafiri wanaotembelea hifadhi za eneo hilo na ndege ambazo hulazimika kurudi jijini. 

Aidha amesema katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali itanunua ndege ndogo abiria ili kuwezeha watalii kufika kwa urahisi katika maeneo ya hifadhiza Taifa.

No comments:

Post a Comment