Na Lorietha Laurence-
Maelezo
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano(Uchukuzi) Mhandisi Dkt. Leornad Chamuriho
ameutaka uongozi wa Bandari unaosimamia Mitambo ya Kupimia Mafuta Nchini (Flow
Meter) iliyoko Kigamboni kutoa taarifa ya kuharibika kwa mitambo hiyo ndani ya
siku mbili.
Hayo yamesemwa leo
jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu huyo alipofanya ziara ya kushtukiza katika
mitambo hiyo na kubaini upungufu katika
vitendea kazi ikiwemo kamera ya kufuatilia mwenendo bandarini hapo, “valvu, sloptank”
na kuchelewashwa kwa ujenzi wa kufunikwa kwa mitambo.
“Ifikapo Jumatatu
nipatiwe taarifa kuhusu matengenezo ya vifaa hivi, hatua zilizochukuliwa na
mnieleze lini ukarabati wake utakamilika” alisema Dkt. Chamuriho.
Aidha, aliongeza kuwa
dhumuni la Serikali ni kuhakikisha vifaa hivyo vinafanya kazi ili kulinda
mapato yatokanayo na mafuta yanayoingia nchini ili Serikali ipate kodi halali
na hivyo kuongeza mapato ya nchi na kuondoa malalamiko kwa wateja.
Naye Meneja Mradi wa
Mitambo ya Kupimia Mafuta kutoka Mamlaka ya
Bandari nchini Mhandisi Mary Mhayaya ameeleza kuwa uharibifu wa vifaa
hivyo umesababishwa na mvua zilizonyesha hivi karibuni na tayari vifaa hivyo vimeanza
kufanyiwa kukabarati.
Kwa upande wake Kaimu
Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Hebel Mhanga amesema ofisi yake
inajukumu la kuhakikisha inatoa huduma sahihi kwa wateja wanaotumia mitambo
hiyo iliyopo bandarini hapo na Serikali
inapata mapato kulingana na huduma iliyotolewa.
Mradi wa Mitambo ya
Kupimia Mafuta nchini ipo katika
majaribio kwa kipindi cha mwaka mmoja ambapo tayari meli tatu zimefanyiwa
majaribio ya upakuaji wa mafuta huku moja ikiwa imefanyiwa vipimo.
No comments:
Post a Comment