Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini Mhe. Peter Kuga Mziray akifafanua jambo wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam . Kulia ni Mhe. Jaji Francis S.K Mutungi, Msajili wa Vyama vya Siasa na Mhe. Vuai Ali Vuai, Makamu Mwenyekiti wa Baraza.
Msajili Msaidizi (Elimu kwa umma na Gharama za uchaguzi) Bi. Piencia C. Kiure akiwasilisha mada ya Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa katika baraza la Vyama vya Siasa lilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Bw. John Cheyo mmoja wa wajumbe wa Baraza la vyama vya siasa akichangia hoja wakati wa kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Picha ya Pamoja ya Wajumbe wa Baraza la vyama vya Siasa baada ya kikao cha Baraza kujadili Mapendekezo ya Mfumo wa utatuzi wa migogoro ndani na baina ya vyama vya siasa kilichofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa GEPF Victoria Jijini Dar es salaam.
Wajumbe
wa Baraza la Vyama vya Siasa Nchini ambalo linaundwa na wawakilishi
wawili kutoka kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu wamekutana mwishoni
mwa wiki katika ukumbi wa mikutano wa GEPF uliopo Victoria Jijini Dar es salam
kujadili mapendekezo ya mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ndani na baina ya vyama
vya siasa .
Mapendekezo
hayo yalitolewa na Mtaalamu wa utatuzi wa Migogoro Bw. Ghalib Galant ambaye
awali alifanya utafiti wa utatuzi wa migogoro ya ndani na baina ya vyama
vya siasa nchini chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama
vya Siasa na kwa udhamini wa UNDP kupitia mradi wake wa
“Democratic Project” ukiwa na lengo la kuiboresha sura namba 258 ya Sheria ya
Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa demokrasia
nchini. Utafiti huo ulishirikisha wadau mbalimbali wa demokrasia ya vyama vingi
nchini vikiwemo vyama vya siasa.
Akiwasilisha
mapendekezo, Msajili Msaidizi Bi. Piencia C. Kiure ,alisema kuwa
ilipendekezwa kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa nchini iweke masharti
yanayohusu utaratibu wa kutatua migogoro ndani na baina ya vyama vya
siasa “ migogoro ndani ya chama ni lazima ishughulikiwe kwanza ndani ya
chama cha siasa na kufikia tamati kwa mfumo wa utatuzi wa migogoro
uliowekwa kwa mujibu wa katiba ya chama, kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi ya
Msajili wa Vyama vya Siasa kwa ajili ya upatanishi” ilikaririwa
sehemu ya mapendekezo
“Upatanishi
ukishindikana mgogoro husika uwasilishwe kwenye Baraza la Uamuzi la
Migogoro ya Vyama vya Siasa kwa uamuzi. Ikiwa muhusika wa mgogoro asiporidhika
na uamuzi wa Baraza la Uamuzi wa migogoro ya vyama vya siasa atawasilisha
mgogoro husika Mahakama Kuu mbele ya Majaji watatu kwa mapitio ya uamuzi wa
Baraza. Muhusika asiporidhika na uamuzi wa Mahakama Kuu, atakata
rufaa Mahakama ya Rufaa” ilifafanua sehemu ya Mapendekezo.
Aidha
kumekuwa na msisitizo wa kufuata mtiririko wa hatua katika utatuzi wa migogoro
kama ilivyobainishwa hapo juu ili kuepusha migogoro ndani ya vyama kwenda
moja kwa moja Mahakamani ambako huchukua muda mrefu na kuathiri
ukuaji wa demockaria ndani na nje ya vyama vya siasa hapa nchini.
Wakichangia
katika mjadala huo, baadhi ya wajumbe walikubaliana na hoja kuwa vyama
vya siasa vitatue kwanza migogoro yake ndani ya vyama na kwamba pale tu
itakaposhindikana ndipo ipelekwe kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Wajumbe
walishindwa kukubaliana katika hoja ya uwepo wa Baraza la Uamuzi wa
Migogoro ya vyama vya siasa, wapo walioona haja ya uwepo wake na wapo
walipendekeza kuwa majukumu ya Baraza hilo yafanywe na Baraza la Vyama vya
siasa lililopo sasa jambo lililosababisha kutokukubaliana katika hoja hiyo.
Pamoja
na michango iliyotolewa , Wajumbe wameishauri Serikali kuona umuhimu wa
kuwekeza katika Baraza la Vyama vya Siasa ili kusaidia utatuzi wa
migogoro nchini kwa kuwa imebainika kuwa machafuko katika nchi nyingi duniani
yamesababishwa na machafuko katika masuala ya siasa.
Akihitaji
ufafanuzi wa hatua gani imefikiwa katika uboreshaji wa Sheria ya Vyama
vya siasa, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama Vya Siasa, Mhe. Peter Kugar Mziray
aliiomba Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutoa ufafanuzi.
Naye
Msajili Msaidizi, Bw. Sisty Nyahoza akitoa ufafanuzi alisema tayari vyama vyote
vya siasa vimeshapelekewa barua vikiombwa kuwasilisha mapendekezo kwa ajili ya
kuboresha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za
Uchaguzi ya mwaka 2010 na kwamba Ofisi inafanya jitihada za kupokea mapendekezo
kutoka kwa wadau wa siasa na ikishakamilisha upokeaji huo, mapendekezo hayo yatawasilishwa
kwenye kamati ya Katiba na Sheria.
No comments:
Post a Comment