Na Jacquiline Mrisho
- MAELEZO
Halmashauri ya Wilaya ya Lindi
iliyopo Mkoa wa Lindi imetenga jumla ya shilingi milioni 162 katika mwaka wa fedha
2016/17 kwa ajili ya kuisaidia shule ya Msingi Nyangao.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bi. Olliver Vavunge alipokuwa akikanusha kuhusu madai
ya wazazi kutaka shule hiyo ifungwe kwa sababu ya ukosefu wa huduma muhimu.
“Kwa kuwa shule hiyo tayari ina
mabweni pamoja na bwalo la chakula, katika bajeti iliyotengwa na Halmashauri kwa
mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi milioni 100 zitatumika katika ujenzi wa uzio wa shule pamoja
na marekebisho madogo madogo ya shule hiyo na shilingi milioni 62 zitatumika kwa
ajili ya chakula”alisema Bi. Olliver
Aidha, Bi. Olliver amekanusha
kupewa bajeti ya shilingi laki tisa kwa ajili
ya matumizi ya shule hiyo kwa mwezi kama ilivyoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo
vya habari na kusema kuwa Serikali inatoa jumla ya shilingi milioni 1.6 kwa kila
mwezi.
Ameongeza kukanusha kuwa si kweli
kuwa wanafunzi wanakula mlo mmoja kwa siku bali wanapata milo yote mitatu kama ilivyo
kawaida.
Shule ya Msingi Nyangao ni shule
ya watoto wenye mahitaji maalumu (walemavu) ambayo hadi sasa ina jumla ya wanafunzi
42 na inahudumiwa na Serikali kwa mahitaji yote.
No comments:
Post a Comment