Monday, April 18, 2016

TAASISI YA GRACA MACHEL MDAU MUHIMU WA ELIMU YA MTOTO WA KIKE NCHINI, IKIWA NA LENGO LA KUIELIMISHA JAMII.

Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

Mtoto huanza kujifunza kulingana na mazingira yake yanayomzunguka, mafunzo hayo yanamuwezesha kupata uzoefu wenye athari ya kujenga akili, tabia ama uwezo wa kimaumbile ili aweze kuyamudu mazingira yake.
Hali hiyo inajenga dhana ya kupata elimu kulingana na mazingira ambayo hujulikana kama elimu isiyo rasmi.
Ni vema ikaeleweka kwamba tunapozungumza kuhusu watoto, tunazikusudia jinsia zote mbili, yaani watoto wa kike na wale wa kiume. Katika hali halisi ndani ya maisha ya kijamii, elimu ni nyenzo ambayo hutumiwa kupitisha maarifa, ujuzi na maadili kutoka kwa kizazi kimoja hadi kingine bila kujali jinsia.
Elimu kwa watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania.
Manufaa hayo ya elimu kwa watoto wa kike yanaweza kuonekana kwa mtu binafsi, familia zao, jamii yote na taifa kwa ujumla.
Ni dhahiri, manufaa yanayopatikana kupita elimu ni mengi katika jamii ikiwemo kupunguza idadi ya watoto ambao wanawake hujifungua, kupunguza idadi ya vifo vya watoto wadogo, kupunguza idadi ya vifo vya akina mama, kuwalinda dhidi ya maambukizo ya VVU/UKIMWI na kuongeza idadi ya wanawake wenye kazi na mapato ya juu ambayo hudumu kwa vizazi vingi.
Hakika ukimuelimisha mtoto wa kike, umemsaidia kuwa na uwezo wa kufanya maamuzi bora kwa manufaa yake, familia yake na hata taifa.
Hali hii imechukua sura mpya nchini Tanzania ambapo Serikali, watu binafsi, mashirika ya dini   na taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu ambayo ndiyo kinga na urithi pekee ambao hawezi kunyang’anywa wala kugawana na mtu mwingine ndani ya familia na hata jamii inayomzunguka.
Sura hiyo mpya imeoneshwa na Mfuko wa Graca Machel (Graca Machel Trust) ambao umejikita katika kusaidia wanawake na watoto nchi kadhaa Barani Afrika.

Taasisi hiyo imebisha hodi na kukaribishwa nchini Tanzania mkoa wa Mara ambapo imeazimia kuwasaidia watoto wa kike 20,000 ndani ya mkoa huo ambao watanufaika kwa fursa ya kupata elimu.
Mapema Aprili 6, 2016 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene alibainisha Mfuko wa Graca Machel umeamua kuwasaidia watoto wa kike wa mkoa wa Mara mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Mama Graca Machel alipomtembelea ofisini jijini Dar es salaam.
Moyo huo na juhudi za kusaidia watoto wa kike ni wa kizalendo ambapo Waziri mwenye dhamana na tawala za mikoa Simbachawene anasema “Ni fursa nzuri ya kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuwasaidia watoto wetu wa kike kielimu ambayo itawasaidia kutoka katika jamii ya umasikini na kuhakikisha wamepata fursa ya kuvuka umri wa vishawishi na maamuzi yasiyo sahihi bila shida na pingamizi lolote”.
Watoto hao wanaotarajiwa kunufaika na Mfuko huo mkoani Mara watatoka katika shule 104. Hatahivyo mfuko huo unatarajiwa kuwafikia watoto wa kike wengi zaidi mara baada ya kuanza kutoa huduma hiyo mkoani humo.
Fursa hiyo adhimu na ni ya kuungwa mkono hasa na wadau wa elimu mkoani Mara na Tanzania kwa ujumla kwani kwa Mama Machel haikuwa lazima kuichagua Tanzania, bali hekima na busara yake inatokana ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji kwa kuzingatia mchango mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo tangu awali.
Uhusiano huo mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili ni wa kihistoria kwani pamoja na harakati za ukombozi  Kusini mwa Afrika, wananchi wa nchi hizo walishirikiana katika shughuli mbalimbali chini ya mwavuli wa unasaba na ushirikiano katika biashara na tamaduni kwenye miji ya Unguja, Kilwa, Lindi na Mtwara kwa upande wa Tanzania na katika miji ya Chilimbo, Tete, Pemba na Sofala nchini Msumbiji.
Jambo jema hakika ni lazima kusifiwa na kushangiliwa ili liweze kufana na kuwa na manufaa mengi zaidi, ndio maana Waswahili husema “Chanda chema huvishwa pete”.
Mama  Machel amekuwa mfano mwema wa kuigwa maana anajali, anathamini na anatambua mchango wa mkoa Mara katika historia ya maisha yake na nchi yake kwa kuwa ndio mkoa alipozaliwa Mwasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeongoza harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika.
Ndiyo maana Mama Machel anasisitiza kwa kusema “Lengo ni kuwabakisha watoto wa kike shuleni ili wapate elimu, ni lazima tusaidiane wote, tuna kila sababu ya kusaidiana”.
Alipokuwa mkoani Mara katika chuo cha ualimu Tarime mapema Mwezi Aprili mwaka huu,   Mama Machel ameitaka Tanzania kuwa na mpango wa utekelezaji katika kuhakikisha wanashughulikia changamoto ambazo zinaweza kuwa sababu za mimba za utotoni kwa wasichana.
Mama Machel alisema kuwa  iwapo Tanzania na nchi nyingine za Afrika watu wataungana  kwa pamoja kila mtu atimize wajibu wake kwa nafasi yake, kwa utaratibu huo wa kujipanga ili kusaidia kundi hilo la wasichana ni hakika mambo yaliyoko mbele yatafanyiwa kazi vilivyo na ndoa za utotoni zitatokomezwa.
Mama Machel alisema kuwa watoto wa kike wanatakiwa kupata nafasi ya kusoma na sio kuolewa wakiwa na umri mdogo, hivyo Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha inakuwa bega kwa bega kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki zake za msingi zikiwamo za elimu.
“Katika mapambano yoyote, kitu kikubwa na cha msingi ni elimu! Elimu pekee ndiyo itamaliza mila zote potofu tutafute mbinu mbadala kuhakikisha watoto wanasoma, walimu wawe ni waangalizi wa watoto, asipofika shule mzazi aulizwe maana watoto wote wanajulikana wanakotoka, tunahitaji tuongeze idadi ya watoto wafike hadi elimu za juu”alisema Mama Machel.
Mkuu wa Mkoa wa Mara Magesa Mulongo alimshukuru Mama Machel kwa moyo wake wa kizalendo kwa kuupa heshima mkoa huo kupitia taasisi hiyo.
Akiwa mkoani Mara, wilayani Tarime Mama  Machel alisisitiza jamii iondokane na suala la ukatili wa kijinsia ukiwamo ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni kwa lengo la kumlinda mtoto wa kike na kumpa nafasi ya kutimiza ndoto zake.
Hatua hiyo ilitokana na Mama Machel kujionea hali ilivyokuwa katika Shule ya Msingi Masanga ambapo alizungumza na wananchi, wanafunzi na mabinti waliokimbia ukeketaji katika msimu wa tohara na kuhifadhiwa kwenye Kituo cha Termination Of Female Genital Multilation (TFGM) Masanga wilayani Tarime mkoani humo ambacho kimeanzishwa na Kanisa Katoliki katika kumuokoa mtoto wa kike na maswahibu ya minyororo ya mila na desturi zisizofaa.
Katika kuthamini na kuupokea kwa vitendo mchango wa Mama  Machel, Serikali, viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa Mara wamesaini mkataba wa kutekeleza ili kuhakikisha watoto wa kike wanapata elimu.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa dhana ya mtoto wa kike kuchunga mifugo zifutiliwe mbali, kila taasisi imepewa jukumu lake, Serikali kupitia mkoa na halmashauri, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) viongozi wa dini na wananchi.
Pande hizo kila mmoja wamesaini pamoja mkataba wa kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kwa kuziweka pembeni imani potofu ambazo ndio zimekuwa kikwazo kwa mtoto wa kike kupata elimu.
“Halmashauri wanawajibu wa kuhakikisha watoto wanaotambuliwa na wasitoroke katika vituo na shule wanaposoma, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na TAMISEMI wajibu wao ni kuandaa sera zinazombeba msichana asitoroke shuleni, wajibu wa Serikali za mitaa na vitongoji ni kuhakikisha kila mtoto anapata haki yake ya elimu wakati mkoa jukumu lake ni kuhakikisha unafanya uratibu wa wadau wote wanahakikisha mtoto wa kike anapata elimu” alisema Mulongo.
Mtazamo huo wa Serikali na wadau wengine wa elimu unaungwa mkono na Mwakilishi wa Shirika la Mfuko wa Idadi ya Watu la Umoja wa Mataifa (UNFPA), Dkt. Natalia Kanem ambapo aliwahimiza watoto walio katika kituo cha Masanga kutokata tamaa bali waweze kushikilia msimamo wa ndoto zao kwa kushirikiana na wazazi waliopata mabadiliko katika kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Aliongeza kuwa mwaka 2014 ulikuwa ni mwaka wa matumaini baada ya wazee wa mila kusema wameondokana na vitendo vya ukeketaji ikiwa ni pamoja na wavulana kufanyiwa tohara.
Mwakilishi huyo alisema vyombo vya kisheria vya mahakama pamoja na polisi vitaendelea kupewa mafunzo juu ya kupinga vitendo hivyo kwa lengo la kuvikomesha kabisa.
“Tanzania ni nchi ndogo na idadi ya watoto waliochini ya miaka 17 ni nusu ya Watanzania kwa hiyo hatuna budi kuwalinda watoto hao kwa kuwapenda na kuwathamini,”alisema Dk Kanem.
Juhudi hizo za elimu kwa mtoto wa kike zinachagizwa na Serikali Tanzania ambayo imekusudia kuleta mapinduzi ya kiuchumi ili kuibadili Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Kusudio hilo la Serikali linaongozwa na Sekta ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo kwa kwa mujibu wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mpango wa muda mrefu wa Maendeleo ya Taifa 2011/12 hadi 2024/25, inatarajiwa kuleta maendeleo ya haraka ya rasilimali watu kwa kutayarisha idadi ya kutosha ya Watanzania walioelimika na kupenda kujielimisha zaidi ili kulifanya Taifa lipate maendeleo na kuwa lenye uchumi wa kati na shindani ifikapo mwaka 2025.
Sera hiyo mpya imeweka dira ya elimu na mafunzo nchini ambayo inayojali jinsia zote kupata elimu kwa usawa na kusimamia nchi iwe ya maendeleo endelevu.
Dira hiyo inasimamia uhalisia “Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa” anapaswa kuzingatia utaifa kwanza.
Ili kuhakikisha elimu inawafikia watoto wote, Serikali imeweka bayana katika Sera ya Elimu ya mwaka 2014 yenye lengo la kuwa na usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo. Pia Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo unazingatiwa.
Hapa nchini taasisi binafsi zimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu licha ya mazingira magumu aliyonayo.
Miongoni mwa taasisi za kupongezwa na kuigwa mfano kutokana na kutoa umuhimu wa mtoto wa kike kupata elimu ni ya Graca Machel Trust, Wanawake na Maendeleo (WAMA) inayoongozwa na Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Mama Salma Kikwete, taasisi ambayo inasimamia Shule ya Sekondari WAMA–Nakayama iliyopo Kijiji cha Nyamisati Wilaya ya Rufiji, Mkoa wa Pwani na Shule ya Sekondari ya WAMA- Sharaf iliyopo Mitwero katika Manispaa ya Lindi.
Taasisi nyingine inayosimamia na kutoa elimu kwa mtoto wa kike ni Mama Clementina Foundation (MCF) yenye makao yake makuu mkoani Kilimanjaro inayoongozwa na aliyewahi kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Weruweu Dkt. Maria Kamm.
Taasisi ya MCF inatoa elimu kwa mtoto wa kike kupitia shule za Kilimanjaro Academy iliyopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na  shule ya sekondari ya Wasichana MCF Makambako iliyopo Makambako.
Katika harakati za kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora ili aweze kujitegemea, kujenga familia bora na kuwa mchango chanya katika kujenga taifa imara kiuchumi, taasisi hizo zimeonesha njia ya kuwa nuru ya mtoto wa kike katika kupata elimu.
Sera ya elimu nchini, inasisitiza uwiano wa uandikishaji wa wanafunzi katika elimu ya msingi kwa wavulana na wasichana uwe takribani 1:1, elimu ya sekondari uwe ni 1:0.9 wakati elimu ya juu ni 1:2.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa mwendelezo wa idadi ya wanafunzi kutoka ngazi moja kwenda ngazi inayofuata kwa wasichana uwiano huo umekuwa ukipungua.
Ingawa kiwango cha mdondoko kinaathiri wavulana na wasichana, tathmini inaonyesha kuwa wasichana wana uwezekano mkubwa zaidi wa kukatisha masomo hususan wanapofikia katika madarasa ya juu kuanzia darasa la tano.
Ndiyo maana taasisi za Graca Machel, WAMA na MCF zimeona kuna umuhimu wa kumsomesha mtoto wa kike kwa ushiriki katika fursa za elimu na mafunzo hatua ambayo itawasaidia wasichana kupata nafasi za usimamizi na uendeshaji katika sekta mabalimbali nchini.
Kwa taarifa za mwishoni mwa mwa 2015 jumla ya wanafunzi 503,914 kati ya wanafunzi 518,034 waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016.
Ki uhalisia, idadi ya wanafunzi waliojiunga kidato cha kwanza mwaka huu sawa na asilimia 97.3 ambao wamepata nafasi za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali.
Ili kuhakikisha wanafunzi hawa wanapata elimu inayotarajiwa Serikali imetenga Sh. bilioni 131 kwa ajili ya shughuli za uendeshaji shule, chakula kwa wanafunzi wa bweni na fidia ya ada ya mitihani kwa kipindi cha kuanzia mwezi Desemba mwaka huu hadi Juni mwaka 2016.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo, alisema kati ya wanafunzi waliochaguliwa, wasichana ni 255,843 sawa na asilimia 99.2 na wavulana ni 248,076 sawa na asilimia 97.7
Sura hiyo inaonesha idadi ya wasichana waliojiunga kidato cha kwanza ni kubwa kuliko ya wavulana kwa zaidi ya asilimia 1.5, ongezeko ambalo linaonesha kuwa Tanzania iko kwenye hatua nzuri ya uelewa wa kumpatia elimu mtoto wa kike.
Siyo wanafunzi wote wanaomaliza shule ya msingi, kidato cha nne na kidato cha sita wanajiunga na shule za Serikali, ndio maana taasisi nyingine zinatoa mchango wao katika kuhakikisha watoto wa kike nchini wanapata elimu katika ngazi mbalimbali.
Hatua hiyo ya Tanzania inaungwa mkono na mataifa duniani ndio maana ikaanzishwa Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ili kutambua haki za watoto wa kike na kuimarisha jitihada za kimataifa za kutokomeza unyanyasaji, ubaguzi na ukatili wa kijinsia na tofauti ya fursa za kiuchumi zinaowaathiri zaidi watoto wa kike.
Takwimu zinaonyesha kuwa nchi zinazowaelimisha watoto wa kike kwa usawa huwa na ustawi na maendeleo makubwa zaidi.
Kwa kuwapa watoto wa kike mwaka mmoja wa ziada wa masomo baada ya muda wa wastani katika elimu ya msingi utawaongezea kati ya asilimia 15 na 20 ya kipato chao na mwaka mmoja wa ziada katika elimu ya sekondari utaweza kumuongezea mtoto wa kike kipato chake kwa kati ya asilimia 15 na 25.
Aidha, watoto wa kike walio soma hukawia zaidi kuolewa na kupata watoto, Hali kadhalika, kuna uwezekano mkubwa zaidi kwa wasichana waliopata elimu hapo baadaye kuwa na watoto wenye afya njema na ambao pia watapata elimu nzuri.
Ndio maana Mke wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne Mama Kikwete aliwahi kusema “……. Mtoto wa Mwenzio ni mwanao, tunamaanisha sote tunapaswa kuwajibika kwa ajili ya ulinzi na ubora wa maisha ya watoto toka wakiwa tumboni hadi wanapozaliwa na kusimamia maadili yao wanapoendelea kukua”.
Mama Salma alitoa msisitizo kwa Watanzania  na kuwaasa waache kulaumiana juu ya maadili ya vijana, na kuwaomba warejee malezi ya wazee ili kila mmoja awajibike kumuona mtoto wa mwenzake kuwa ni wa kwake na kumrekebisha pale anapokosea.
Ni wajibu wa kila mpenda maendeleo kujua kuwa ni fursa ya pekee kumuelimisha mtoto wa kike wajibu na dhamana ya jamii kutambua ukimuelisha mtoto wa kike ni kuelimisha jamii nzima. 
Ndiyo maana kauli mbiu ya mwaka huu ya kuadhimisha siku ya wanawake duniani ambayo huadhimishwa kila mwaka Machi 8 imesisitiza kuwa “Usawa kwa wanawake ni maendeleo kwa wote”
Mwisho

No comments:

Post a Comment