Na Magreth Kinabo-
Maelezo
Jamii imeshauriwa kuwapeleka
watoto wote wanaostahili kupata chanjo walio chini ya
umri wa miaka mitano katika vituo vya afya ili waweze kupatiwa chanjo ili
kuweza kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto.
Kauli hiyo ilitolewa
Aprili 27, mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.
Mpoki Ulisubisye wakati wa maadhimisho ya wiki ya chanjo nchini
yaliyofanyika kwenye hoteli ya Serena Jijini Dares Salaam.
Alisema utoaji
wa chanjo hiyo umeaanza Aprili 25 hadi 29 mwaka huu na kaulimbiu ya
mwaka huu ni ‘ Kumilisha Chanjo,Epuka Ugonjwa wa Polio’. Hivyo vituo vya kutolea huduma za afya vinafunguliwa kuanzia saa 2: 00 asubuhi
hadi saa 11.00 jioni.
“ Kila mmoja wetu
anawajibu wa kuhakikisha mtoto wake , mtoto wajirani au mlengwa
mwingine yeyote anapewa haki ya chanjo ili kumzuia asipatwe na maradhi ambayo
yanakingwa na chanjo au asiwe na hatari kwa wengine kwa kuwaletea ugonjwa,”
alisema Dkt. Ulisubisye.
Aliongeza kuwa chanjo ni
mikakati muafaka katika kutokomeza maradhi na kupunguza vifo vya watoto, hivyo
hupunguza gharama kubwa ambazo familia zetu na taifa kwa ujumla
lingetumia katika kutibu maradhi yanatokana na magonjwa yanayozuilika kwa
chanjo.
Alisema chanjo huzuia
takribani vifo milioni mbili hadi tatu kwa kila mwaka kutokana na
maradhi yanayokingwa kwa chanjo duniani.
Aliyataja maradhi hayo
kuwa ni Dondakoo, Surua ,Polio,Kifua Kikuu,Kifaduro,PepoPunda,Homa ya
ini,homaya uti wa mgongo,kichomi na kuhara.
No comments:
Post a Comment