Sunday, April 24, 2016

MAALIM SEIF AENDELEA KULIA NA KIKWETE KWA KUPINDUA MATOKEO UCHAGUZI MKUU WA ZANZIBAR.


Katibu Mkuu wa CUF, Seif Sharif Hamad ameendelea kumtupia lawama Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akidai kuwa alitumia dola ‘kupindua’ demokrasia ili kuinusuru CCM iliyokuwa imebwagwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita.

Alisema Kikwete ambaye wakati huo alikuwa Amiri Jeshi Mkuu, anastahili lawama kwa madai kuwa alituma vyombo vya dola kugeuza uamuzi wa Wazanzibari waliokuwa wameufanya kupitia masanduku ya kura Oktoba 25 mwaka jana.

Maalim Seif aliyasema hayo jana pale wananchi walipomtaka kutoa neno la kuwasalimu alipopita katika Msikiti wa Ijumaa wa Masjid Swahaba, Mtoni Garagara, Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.

“Kilichofanyika si kitendo cha kiungwana hata kidogo, ni uhuni wa hali ya juu uliopangwa kwa makusudi na watu wasioitakia mema Zanzibar na hivyo wakaamua kutoheshimu haki na uamuzi halali wa wananchi,” alisema.

Maalim Seif alisema nchi ni mali ya wananchi ambao siku zote watabaki kuwa sehemu muhimu ya uamuzi wa nani awaongoze.

Katibu mkuu huyo ambaye alikuwa mgombea wa urais wa Zanzibar katika uchaguzi huo, alisema watawala wanapaswa kutambua wananchi ndiyo huamua watu wanaowataka na siyo mabavu ya kulazimisha kwa kutumia dola au majeshi.

Hata hivyo, Maalim Seif alisema anaelewa hali ilivyo katika jamii na pia katika mioyo za Wazanzibari ambao uamuzi wao ulipinduliwa.

Maalim Seif aliyedai kushinda nafasi hiyo, aliwataka Wazanzibari kuendelea kuwa watulivu wakielewa kuwa wao ndiyo washindi na ushindi hautapotea.

Mwanasiasa huyo alisema juhudi zinaendelea kuhakikisha haki ya uamuzi wao kupitia masanduku ya kura inapatikana.

Wananchi walioibuka kwa wingi katika eneo hilo baada ya kubaini sauti iliyokuwa ikizungumza kwenye kipaza sauti ni ya Maalim Seif, walielezea kufurahishwa na kiongozi huyo.

“Tumejisikia furaha angalau kusikia sauti ya simba wa nyika, Maalim Seif akinguruma,” alisema mkazi wa Mtoni Kidatu, Bura Juma.

Slim Said alisema: “Unajua Maalim ni kipenzi cha watu, sasa ukimsikia tu unaondoka na hisia za matumaini.”

Msafara huo wa Maalim usiokuwa na king’ora kama ilivyozoeleka ulionekana ukiingia taratibu, hali ambayo haikuamsha shangwe mwanzoni kabla ya watu kupashana habari na hatimaye kujaa mahali alipokuwa.

Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulitawaliwa na mvutano wa kisiasa visiwani Zanzibar baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo akidai kuwa sheria na taratibu zilivunjwa. Kutokana na hatua hiyo, baadaye Jecha alitangaza uchaguzi wa marudio Machi 20 mwaka huu ambao uligomewa na vyama 10 kati ya 14 vilivyoshiriki uchaguzi wa awali.

Katika uchaguzi wa marudio, Dk Ali Mohamed Shein alishinda kwa asilimia 91.4.

No comments:

Post a Comment