Thursday, April 14, 2016

DK. KIGWANGALLA AKUTANA NA AFISA MIRADI KUTOKA SHIRIKALA LA KIMATAIFA LA NGUVU ZA ATOMIKI (IAEA)


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla (wa pili kushoto) akisikiliza kwa makini mazungumzo na Afisa miradi anayesimamia miradi ya mionzi barani Afrika kutoka wakala wa Kimataifa wa nguvu za Atomiki (IAEA), Bw. Solomon Haile (wa kwanza kulia). Wengine ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayeshughulikia magonjwa yasiyo ambukiza, Profesa Ayoub Magimba (katikati), akifutiwa na Mkurugenzi taasisi ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaisalage na kushoto Mratibu wa Magonjwa ya Saratani Kitaifa pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kwa watu wazima, Dk. Sara Maongezi. (Picha na mpiga picha wetu).

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla amekutana na Afisa miradi anayesimamia miradi ya mionzi barani Afrika kutoka wakala wa Kimataifa wa nguvu za Atomiki (IAEA), Bw. Solomon Haile katika mazungumzo yaliyofanyika leo asubuhi Aprili 14.2016, Ofisini kwake jijini Dar es Salaam. 
Katika mazungumzo hayo, Dk. Kigwangalla ameomba Tanzania ipatiwe kibali cha kununua mashine mpya ya kutibu saratani (LINAC) Sambamba na sehemu ya msaada iliyoahidiwa na Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Bw.Yukiko Amano mbele ya Waziri Mkuu Mstaafu, Mh. Mizengo Kayanda Pinda miaka mitatu iliyopita.

Tanzania tayari imetenga kiasi cha Euro 1.65 Milioni kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya mchango wake kwa asilimia 50 kama mradi ulivyokuwa awali.Mh. Kigwangalla alisema: “Bahati mbaya sana kutokana na ucheleweshwaji, Bajeti ya msaada huo kutoka IAEA ilipitwa na wakati na kusababisha Tanzania kukosa fursa hiyo. Malengo ya Tanzania ni kununua mashine hizo mbili kwa ajili ya kuboresha huduma za tiba ya Mionzi nchini”.

Ujenzi wa jengo kwa ajili ya kufunga mashine hizo mbili umesha kamilika na mashine moja itakamilika mwaka huu na ya pili mwakani ili kuboresha huduma za Saratani nchini.

Katika mazungumzo hayo, Maafisa waandamizi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Woto walishiriki, akiwemo Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba anayeshughulikia magonjwa yasiyo ambukiza, Profesa Ayoub Magimba, Mratibu wa Magonjwa ya Saratani Kitaifa pamoja na magonjwa yasiyoambukiza kwa watu wazima, Dk. Sara Maongezi pamoja na Kaimu Mkurugenzi taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Julius Mwaiselage.

No comments:

Post a Comment