Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akizungumza na Waganga, Wauguzi na
wafanyakazi wa Hospitali ya Mkoa wa Mtwara wakati alipoitembelea Februari 29,
2016.
·
Ni baada ya kudai rushwa ya sh. 100,000/- kumfanyia
upasuaji mgonjwa.
·
Mama alilazimika kuuza shamba ili apate fedha za
kumtibia baba yake
·
Aagiza maduka ya dawa nje ya hospitali hiyo yafungwe
leo hii
·
Amwagiza RAS aitishe kikao cha watumishi wote leo
saa 9 alasiri
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza kusimamishwa kazi kwa Dk. Fortunatus
Namahala wa kitengo cha upasuaji katika hospitali ya Ligula ambayo ni hospitali
mkoa wa Mtwara kutokana na tuhuma za kumdai mgonjwa rushwa ya sh. 100,000/-.
Pia ametoa agizo la kufungwa kwa maduka yote ya dawa yaliyo nje ya
hospitali hiyo kuanzia leo na kumtaka Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Alfred
Luanda asimamie zoezi hilo mara moja.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Februari 29, 2016) kwenye kikao cha
watumishi wa hospitali hiyo alichokiitisha baada ya kutembelea maeneo kadhaa ya
hospitali hiyo na kupokea malalamiko kutoka kwa wagonjwa na ndugu wenye
wagonjwa waliolazwa.
Mara baada ya kuwasili, Waziri Mkuu aliamua kwenda mojamoja mapokezi
badala ya wodini kama alivyopangiwa na kuuliza maswali ni kwa nini wana dirisha
moja la kupokelea wagonjwa wote. "Dirisha la wazee lipo?" akajibiwa
hakuna. "Dirisha wa watu wa Bima ya Afya (NHIF) lipo" nalo pia
akajibiwa halipo. "Je wazee wana daktari wao", hakupata jibu.
"Mganga Mkuu ni kwa nini hujatenga dirisha la wazee wakati haya
maelekezo yalishatolewa siku nyingi? Tengeni dirisha la wazee na
uhakikishe wana daktari wao. Siyo kuwaleta huku ili waje kusukumana na wagonjwa
vijana," alisema wakati akimwagiza Mgaga Mkuu wa Mkoa huo, Dk.
Shaibu Maarifa.
Akiwa njiani kuelekea wodi aliyopangiwa kuiona, Waziri Mkuu alikutana na
kundi la wagonjwa waliokuwa wakiimba "tuna jambo, tuna jambo"
wakiashiria kutaka kusikilizwa. Kati ya wauguzaji watatu aliowasikiliza, Waziri
Mkuu alipokea kero za kuuziwa dawa kwa bei za juu kwenye maduka ya dawa
binafsi, lugha mbaya za madaktari na wauguzi, uchafu wa vyoo na uhaba wa maji.
Lakini kero ya Bi. Tatu Abdallah aliyelazimika kuuza shamba la baba yake
ekari 2.5 ili apate fedha za kulipa gharama za kufanya upasuaji kwenye
hospitali binafsi baada ya baba huyo kutimuliwa kutoka hospitali ya Ligula
ndiyo ilimgusa zaidi Waziri Mkuu.
"Februari mosi nilimleta baba yangu hapa nikaambiwa anatakiwa
kufanyiwa upasuaji. Nikaandikiwa ninunuue dawa za sh. 85,000/- hapo nje
(pharmacy haikumbuki jina) pia uzi wa kushonea kwa sh. 25,000/-. Lakini pia
daktari akasema anataka sh. 100,000/- ya kwake. Lakini hadi Februari 7
hakufanyiwa huo upasuaji."
"Tarehe 12 Februari baba alitolewa wodini na kuambiwa arudi
tarehe 16 Februari. Niliumia sababu kijiji tunachotoka ni mbali na hali ya baba
ilizidi kuzorota. Ndipo baba akaniambia nirudi kijijini kwetu Kilomba nikauze
ekari 2.5 za shamba lake ili tulipie matibabu. Niliuza na kumpeleka baba katika
zahanati ya Sajora. Huko nililipa sh. 560,000/- na baba akafanyiwa upasuaji
sasa hivi yuko nyumbani".
"Leo nataka huyu daktari aje achukue boksi hili la dawa
alizoniandikia na pia anirudishie hela yangu iliyopotea bure. Mie sijazitumia,
ni kwa nini aliniandikia wakati baba hajampa huduma yoyote?" Alipoulizwa
kama anaweza kumtambua akimuona, mama huyo alikiri kuwa anaweza.
Waziri Mkuu alitembelea pia wodi ya akinamama waliojifungua na kukuta
wakiwa wametandikiwa shuka moja na wagonjwa kulazimika kuweka khanga juu ya
mipira wanayolalia wodini ambayo pia wanaambiwa wajinunulie kabla ya kwenda
hospitali kujifungua.
Akiwa njiani kuelekea theatre, Waziri Mkuu alipata kilio cha
wagonjwa wengine ambao walisema hospitali hiyo haina maji, choo kinachotumika
ni kimoja na kwamba usafi umefanyika leo waliposikia kuwa atatembelea hospitali
hiyo.
Akiwa katika kikao na watumishi hao, Waziri Mkuu aliwainua madaktari wote
ili wajitambulishe ndipo akamuomba mama aliyedaiwa rushwa aende kumshika mkono
daktari mhusika.
"Gwaride la utambuzi ni jambo la kawaida. RPC hakikisha huyu mama
hasumbuliwi. Lakini leo nitaanza na huyu Daktari kwa sababu rushwa haivumiliki.
RAS simamia suala lake lakini pia shirikiana na TAKUKURU na Polisi kufanya
uchunguzi wa jambo hili hadi mwisho," alisema.
Kuhusu madai na stahili za watumishi, Waziri Mkuu amemwagiza RAS,
RMO na Afisa Utumishi wa mkoa wafanye kikao na watumishi wote wa hospitali hiyo
leo saa 9 alasiri na kisha wamletee taarifa.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kumsimamisha Dk. Namahala, Waziri Mkuu
alitumia muda mwingi kuwaelezea watumishi hao jinsi walivyo na umuhimu katika
huduma zao na kwamba nafasi yao ni nyeti kwa maisha ya binadamu hivyo wanapaswa
kuwa na huruma na siyo kuwaumiza wananchi wa kipato cha chini ambao hawana
uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Aliwataka waache tabia ya kuwatoza fedha watoto wanaolazwa hospitalini
hapo na wanawake wanaojifungua kwani wanapaswa kutibiwa bure kwa mujibu wa sera
ya Serikali.
Sakata la hospitali ya Ligula lilianza juzi (Jumamosi, Februari 27, 2016)
wakati Waziri Mkuu akiwahutubia mamia ya wakazi wa Mtwara kwenye mkutano wa
hadhara uliofanyika katika uwanja wa mashujaa ambapo baadhi yao walikuwa
wakichomekea kuwa aende hospitalini hapo kwa kuwa kuna majipu ya kutumbua.
Waziri Mkuu aliwajibu kuwa amesikia ujumbe wao na ataenda huko lakini
alishindwa kutokana na ratiba za siku hiyo kumalizika jioni sana.
No comments:
Post a Comment