Thursday, March 17, 2016

CUF WATOA TAMKO JIPYA WAMPINGA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI ALIYESEMA KUWA KUNA AMANI YA KUTOSHA ZANZIBAR:

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) , Magdalena Sakaya akionyesha picha ya mhanga wa vipigo zanzibar.


WAKATI uchaguzi wa marudio ukitarajiwa kufanyika jumapili visiwani Zanzibar, Chama Cha Wananchi (CUF) kimesema kuwa haki za binadamu zimeendelea kuminywa kwa kiasi kikubwa visiwani humo huku wafuasi wa chama hicho wakilengwa zaidi.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) , Magdalena Sakaya, ambaye pia ni mbunge wa viti maalum, ameyasema hayo leo wakati alipozungumza na waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Ofisi za Chama hicho zilizopo Buguruni  jijini hapa.

Magdalena amesema kuwa Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa ya haki za binadamu hivyo mambo yanayotokea Zanzibar ni ya kushangaza na hayapaswi kufumbiwa macho kwa ustawi wa Taifa.

Amesema kuwa baada ya CUF kutangaza kujitoa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi wa marudio , wananchi wa Zanzibar wamekuwa wakiishi kwa hofu huku vikundi vya matukio ya uhalifu maarufu’mazombi’ yakipiga watu pasipo na kuchukuliwa hatua zozote na vyombo vya usalama.

“Mara kwa mara tumekuwa tukiwaambia jeshi la polisi kuhusiana na haya mazombi ila cha kushangaza hadi leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kuhusiana na kukamatwa kwa makundi hayo ya mazombi,”alisema.

Chama hicho kimesema kuwa viongozi wao kadhaa wamekamatwa kwa nyakati tofauti ambapo jana Mkurugenzi wa Habari na Uenezi Taifa -Hamad Masoud, alikamatwa na kuwekwa kizuizini na Polisi baada ya kutoa taarifa ya matukio mbalimbali yanayoendelea visiwani humo ambayo ni ya kinyume na haki za binadamu.

“Jambo la kushangaza kila tukio baya likitokea wanasingiziwa wafuasi wetu, mara kwa mara wamekuwa wakikamatwa na tangu januari hadi sasa zaidi ya wafuasi 60 wamekamatwa kwa madai ya kuhusika na uvunjifu wa amani,”alisema.

“Sisi tumeamua kujitoa kwenye uchaguzi huo ili wananchi wetu wawe huru na kuwaepusha kwenye vurugu, kwa hiyo
Chama cha Mapinduzi kisiwalazishe wananchi kufanya mambo ambayo wenyewe hawako tayari kuyafanya na kuyaona ni kinyume na Katiba, kwa sababu uchaguzi huo wa marudio ni haramu.

“Asilazimishwe mbuzi kunywa maji wakati hana kiu,”alisema Magdalena na kuongeza kuwa wangetegemea uchaguzi huo kufanyika kwa amani baada ya kutangaza kujitoa mapema mwaka huu.
Magdalena alisema kuwa yapo maeneo kadhaa visiwani humo wananchi wamepigwa marufuku ya kutoonekana wakitembea kuanzia saa mbili usiku hatua inayosababisha hata wengine kushindwa kwenda kufanya ibada.

Akizungumzi kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ya kusema kuwa hakuna watu wanaopigwa visiwani humo, Kiongozi huyo wa Chama alipinga madai hayo na kusema kuwa ni hatari kuudanganya umma kwa kuficha ukweli na kuacha watanzania wateswe.

Aliishauri Serikali kuhakikisha kuwa usalama wa wananchi visiwani humo unaimarishwa kwa kufuata misngi ya haki za binadamu na utawala bora, pia ichukue hatua dhidi ya ‘mazombi’ ambayo yamekuwa yakiripotiwa kupiga watu kwa nyakati tofauti. 

No comments:

Post a Comment