Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu ametoa Rai kwa wamiliki wa vituo binafsi vya kutoa huduma za afya kupanua wigo wa huduma na kutoa matibabu ya Kifua Kikuu katika taasisi zao.
Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri huyo wakati akitoa tamko katika kuadhimisha siku ya Kifua Kikuu duniani ambapo ufanyika tarehe 24 Machi kila mwaka.
“Pamoja na ushiriki mzuri katika kutoa huduma mbalimbali za afya, napenda kutoa rai kwa wamiliki wa vituo binafsi vya afya vya kutoa huduma ya afya kupanua zaidi wigo wa huduma na kuanza kutoa matibabu ya Kifua Kikuu katika taasisi yenu” Alisema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo itatoa ushirikiano kwa kuwapatia vifaa na dawa za matibabu ya ugonjwa wa Kifua Kikuu ili kuhakikisha vituo binafsi vinatoa huduma iliyo bora.
Aidha Ummy ameongeza kuwa Mikoa inayoongoza kwakuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu ni pamoja na Arusha, Dar es Salaam, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Shinyanga na Tanga.
“Takwimu za mwaka 2015 zinaonyesha kuwa mikoa hii inachangia zaidi ya asilimia 60% ya wagonjwa wa Kifua Kikuu waliogundulika Tanzania Bara na Visiwani” aliongeza Waziri Ummy.
Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi kuwa na kawaida ya kufanya uchunguzi wa afya ili kuweza kugundua tatizo mapema na kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu nchini kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza uwezekano wa kupata maambukizo mapya ya Kifua Kikuu katika jamii.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema “Tuungane kutokomeza Kifua Kikuu” ambapo inaweka msukumo wa kipekee kwa nchi kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya Kifua Kikuu.
No comments:
Post a Comment