BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imekuwa ikifuatilia kwa makini majadiliano
yanayoendelea katika mitandao mbalimbali ya kijamii kufuatia video iliyotumwa
katika YouTubehttps://www.youtube.com/watch?=iveX49WE7fw na
imekuwa ikisambazwa kupitia njia mbalimbali za habari ikimuonesha mtu mmoja
kutoka nchi jirani akisema kuwa Olduvai Gorge ambayo kimsingi iko Tanzania
kwamba iko Kenya.
Video hii imeibua majadiliano katika mitandao ya kijamii baina ya
watanzania na watu wengine ambao wanaitakia mema Tanzania na wanaoelewa vizuri
kuwa Olduvai Gorge iko Tanzania.
Bodi ya Utalii Tanzania kama taasisi ya Umma yenye jukumu la kuvitangaza
vivutio vyetu vya utalii imeshtushwa na video hii iliyojaa upotoshwaji mkubwa
ambao tunaamini mbali ya malengo mengine inalenga kuchafua kazi nzuri ambayo
imekuwa ikifanywa na Bodi kwa kushirikiana na wadau wengine katika kutamgaza
vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Olduvai Gorge.
Tunapenda kuchukua fursa hii kupinga vikali upotoshwaji huu uliofanywa na
mtu huyo wakati akihutubia mkutano amabao tumeambiwa ulikuwa ni wa Vijana wa
Umoja wa Mataifa uliofanyika Amerika mwezi Agosti mwaka jana. Tunapenda dunia
ifahamu kuwa kama ilivyo kwa Mlima Kilimanjaro, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,
Zanzibar n.k Olduvai Gorge mahali panapoaminika kuwa ndipo binadamu wa kwanza
duniani aliishi na ambako Dr. Louis na Mary Leakey waligundua fuvu la binadamu
huyo wa kale anayesadikiwa kuishi miaka takribani milioni 2 iliyopita iko pia
Tanzania na si mahali pengine popote duniani. Eneo hili la Olduvai Gorge liko
katika bonde la ufa katikati ya bonde la Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti mkoani Manyara nchini Tanzania.
Tunatoa wito kwa watanzania mahali popote walipo kuendelea kuunga mkono
juhudi za Bodi ya Utalii Tanzania za kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya
Utalii kwa kujibu na kusahihisha papo hapo bila woga mara tu taarifa ya
upotoshaji kuhusu nchi yetu inapotolewa iwe ni kwenye mikutano ya ndani ya nchi
au ya Kimataifa. Tunaamini kuwa ni jukumu la kila mtanzania kuitangaza Tanzania
na vivutio vyake vya Utalii badala ya kuiachia TTB kazi hii peke yake.
Yawezekana katika mkutano huo wa vijana ambao mjumbe huyo wa nchi jirani
alipata fursa ya kuzungumza na kufanya upotoshaji huzo, wajumbe wa Tanzania pia
walikuwepo ambao wangweza kukosoa upotoshaji huo papo hapo na kuelezea ukweli
na usahihi wa mahali ilipo Olduvai Gorge.
Imetolewa na:
Ofisi ya Uhusiano
BODI YA UTALII TANZANIA.
No comments:
Post a Comment