Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un ametangaza kwamba taifa hilo litafanyia majaribio silaha za nyuklia na makombora ya masafa marefu karibuni.
Amesema majaribio hayo yataimarisha uwezo wa taifa hilo kutekeleza mashambulio ya nyuklia, vyombo vya habari vya serikali nchini humo vimeripoti.
Kim Jong-un ametoa tangazo lake la karibuni zaidi alipokuwa akiongoza maonesho mwigo ya teknolojia ambayo inahitajika kuwezesha kombora lenye kilipuzi cha nyuklia kuingia tena ardhini baada ya kurushwa anga za juu, shirika la habari la KCNA limeripoti.
Shirika hilo limemnukuu akisema majaribio hayo yatafanyika “karibuni” lakini hakusema ni lini.
Korea Kaskazini imekuwa ikitoa msururu wa vitisho baada ya kuwekewa vikwazo vipya na Umoja wa Mataifa.
Lakini ingawa inajulikana kuwa ina silaha za nyuklia, wengi wanashuku uwezo wake wa kuzitumia.
Wiki iliyopita, Bw Kim alidai wanasayansi wa taifa hilo walikuwa wamefanikiwa kuunda kilipuzi cha nyuklia kidogo sana ambacho kinaweza kuwekwa kwenye makombora ya masafa marefu.
- Mashirika ya habari ya serikali yalitoa picha ambazo zilidai kuonesha kilipuzi hicho.
Wizara ya ulinzi ya Korea Kusini imesema inatilia shaka madai ya Kaskazini na kusema haiamini taifa hilo limeweza kugundua teknolojia ya kuwezesha vilipuzi kuingia tena ardhini kutoka anga ya juu.
Mnamo Jumanne, Rais wa Korea Kusini Park Geun-hye alionya kuwa iwapo Korea Kaskazini itaendelea na “uchokozi” na iwapo haitabadilisha msimamo wake basi inafuata njia ya kujiangamiza.
Mwezi Januari, Korea Kaskazini ilifanya jaribio lake la nne la nyuklia, na kusema lilikuwa bomu lenye nguvu sana la haidrojeni.
Hilo lilifuatiwa na kuzinduliwa kwa setilaiti kwa kutumia teknolojia ya makombora ambayo imepigwa marufuku.
Matukio yote mawili yalikiuka vikwazo vilivyowekwa vya Umoja wa Mataifa.
Katika wiki moja iliyopita, vikosi vya Marekani na Korea Kusini vimekuwa vikifanya mazoezi ya pamoja ambayo ndiyo makubwa zaidi kufanywa na nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment