Msimamizi wa ujenzi wa Mradi wa bomba jipya la maji kutoka Ruvu Juu Mlandizi hadi Dar es salaam lenye urefu wa km 40 ambalo liko katika hatua za mwisho za ujenzi kutoka DAWASA Mhandisi Christian Gava akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiufundi kuhusu mradi huo. Kushoto ni Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Jamii wa DAWASA Neli Msuya.
Msimamizi wa ujenzi wa Mradi wa bomba jipya la maji kutoka Ruvu Juu Mlandizi hadi Dar es salaam lenye urefu wa km 40 ambalo liko katika hatua za mwisho za ujenzi kutoka DAWASA Mhandisi Christian Gava akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiufundi kuhusu mradi huo.
Moja ya daraja linapopitisha bomba hilo kutoka Ruvu Juu Mlandizi hadi Dar es salaam lenye urefu wa km 40 linavyoonekana mara baada ya kukamilika eneo la Kibamba.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Jamii wa DAWASA Bi. Neli Msuya akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu ujenzi wa bomba hilo.
Wataalam wa ujenzi kutoka DAWASA na kampuni ya Megha Engineering & International Ltd inayojenga bomba jipya la maji kutoka Ruvu Juu Mlandizi hadi Dar es salaam India wakiangaliamoja ya matoleo 12 yanayopita chini ya barabara kuu ya Morogoro eneo la kimara.
Waandishi wa Habari, Wataalam kutoka DAWASA nakutembelea eneo Kimara na Kibamba ambako mafundi wa Kampuni inayojenga mradi huo ya Megha Engineering & International Ltd wakiangalia umaliziaji wa ulazaji wa bomba la maji.
Na.Aron Msigwa - MAELEZO.
Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam ( DAWASA) imesema kuwa wakazi zaidi wa jiji la Dar es salaam na Kibaha mkoani Pwani wanatarajia kunufaika na huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama ifikapo Juni mwaka huu kufuatia mradi wa ujenzi wa bomba jipya la maji kutoka Ruvu Juu Mlandizi, Kibaha hadi jijini Dar es salaam kuwa katika hatua za mwisho za ujenzi.
Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa Jamii wa DAWASA Neli Msuya ameyasema hayo leo jijini Dar es salaam mara baada ya kutembelea eneo Kimara na Kibamba ambako mafundi wa Kampuni inayojenga mradi huo ya Megha Engineering & International Ltd kutoka India wanaendelea na kazi ya ujenzi wa madaraja na matoleo ambayo bomba hilo linapitia katika barabara ya Morogoro.
Amesema hadi kukamilika kwake mradi huo utagharimu kiasi cha dola za Kimarekani milioni 59.3 na utawezesha kiasi cha Lita milioni 196 za maji kusafirishwa kwa siku ambazo zitaongezwa kwenye lita milioni 270 zinazozalishwa kwa siku na Mtambo wa Maji wa Ruvu Chini ulioko Bagamoyo mkoani Pwani.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kabisa tatizo la uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es salaam ambayo yameunganishwa na mtandao wa mabomba ya DAWASCO ambayo yalikua hayapati maji kwa muda mrefu au kupata kwa mgawo kufikia mwezi Juni, 2016.
Bi. Neli amesema kuwa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika katika kipindi kilichopangwa na kuanza kuwanufaisha wananchi, ujenzi wake unakwenda sambamba na umaliziaji wa tenki jipya la kuhifadhia maji lililoko eneo la Kibamba lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita milioni 10 ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.
Aidha, amesema kuwa kazi ya ukarabati wa matenki ya zamani yaliyoko eneo la Kimara jijini Dar es salaam inaendelea sambamba na ubadilishaji wa mifumo ya mabomba ya zamani ambayo sasa ni chakavu ili iweze kuhimili wingi wa maji uliopo.
" DAWASA tumeshaingia mkataba na Mkandarasi kwa ajili kulaza upya mabomba ya maji kwa wananchi wasiounganishwa na maji ili waweze kuingia kwenye mtandao wa mabomba yetu, kazi hii inaendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kimara, Mlandizi,Kibaha, Kwembe, Segerea, Changanyikeni, Mbezi na Makuburi" Amesema.
Bi. Neli ameongeza kuwa baadhi ya maeneo yataanza kupata mabadiliko ya huduma ya maji kuanzia mwezi Mei kufuatia maji yatakayosukumwa kutoka Ruvu, Mlandizi kuanza kutoka katika kituo cha kwanza kwenye tenki la maji la Kibamba.
“Tunatarajia wananchi waliounganishwa na mtandao wataanza kuona mabadiliko kuanzia mwezi Mei, japo sasa kuna maeneo yana mgawo wa Dawasco,lakini baada ya maji haya kufika na kuanza kutoka kwenye kituo cha tenki la Kibamba wananchi watakua na maji ya kutosha" Amesisitiza.
Kwa upande wake Msimamizi wa ujenzi wa Mradi huo kutoka DAWASA Mhandisi Christian Gava akitoa ufafanuzi wa masuala ya kiufundi kuhusu mradi huo amesema kuwa ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo imewalazimu kujenga maungio 15 ambayo bomba hilo linavuka mito na matoleo 12 yanayopita chini ya barabara kuu ya Morogoro.
Amesema kazi ya wekaji wa miundombinu ya kulifanya bomba lipite juu ya mto kupitia madaraja yaliyojengwa imefanyika kwa umakini mkubwa ili kuepuka kuathiri uasili wa mito husika.
Aidha, amesema kuwa ili kulinda bomba hilo na athari za mafuriko katika mito hiyo ulifanyika utafiti maalum ukihusisha upimaji wa kimaabara wa udongo ili kubaini namna udongo huo unavyoweza kubeba nguzo kubwa zilizoshika bomba hilo.
Mhandisi Gava ameongeza kuwa ujenzi wa tenki la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 umekamilikia kwa 98 na kubainisha kuwa kilichobakia ni umaliziaji wa kazi ndogondogo.
“Ujenzi wa Tenki umekamilika, hatua inayofuata ni kukamilisha kazi ndogondogo kisha kulijaza maji kama sehemu ya uangalizi na taratibu za kiufundi, Tunatarajia wiki ijayo tutajaza maji" Amesisitiza Mhandisi Gava.
No comments:
Post a Comment