Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jana imezifungua ofisi za Kampuni maarufu ya uwakili ya Mbunge wa Butiama, Nimrod Mkono, ikiwa ni siku chache baada ya kuzifungia kwa madai kuwa kampuni hiyo inadaiwa kodi ya shilingi bilioni 1.
TRA waliwasili katika jengo la ofisi hizo zilizoko katika jengo la Bank ya Exim iliyoko jijini Dar es Salaam (ingawa ilikuwa sikukuu), pamoja na Kampuni ya udalali ya Yono na kuzifungua ofisi hizo mbele ya Nimrod Mkono na binti yake.
Mkurugenzi wa huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo amekiri kufunguliwa kwa ofisi hizo. Kayombo amesema kuwa uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuwepo kwa makubaliano kati ya pande mbili na ahadi ya kufanya malipo iliyowekwa na mkono.
“Ni kweli muda upo tuliokubaliana lakini hatutaki uwe katika vyombo vya habari, kutokana na nia ya dhati aliyoonesha Mkono ndio maana tumekubaliana nae,” Kayombo anakaririwa.
Hatua hiyo imefikiwa huku kukiwa na taarifa kuwa ingawa Mkono amefungiwa ofisi zake akidaiwa kodi ya shilingi bilioni 1, yeye anaidai Serikali takribani shilingi bilioni 9 kwa kazi alizofanya ndani ya Tanzania Bara na Zanzibar.
No comments:
Post a Comment