Watafiti wa mambo ya kale nchini Israel wamegundua makaburi ya kwanza ya Wafilisti.
Makaburi hayo, yaliyopatikana eneo la Ashkelon, yaligunduliwa mwaka 2013, lakini habari hizo zilifichuliwa Jumapili.
Habari hizi ziliwekwa siri muda huo wote kuzuia kushambuliwa na waandamanaji wa makundi ya Wayahudi wahafidhina ambao hawakutaka makaburi hayo yafukuliwe.
Taarifa zinasema ugunduzi huo huenda ukafichua mengi kuhusu asili ya Wafilisti ambao wamezungumziwa sana katika vitabu vya kidini.
Mafanikio hayo yalitokea mwisho wa mwaka wa 30 wa uchimbaji ulioongozwa na kundi la Leon Levy Expedition.
Viongozi wa uchimbaji huo wanasema walipata makaburi yaliyozingirwa na manukato, vyakula, mapambo, vito na silaha.
Yanadaiwa kujengwa na kutumiwa kati ya karne ya 11 na karne ya 8 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu.
"Baada ya kutafiti kuhusu Wafilisti kwa miongo mingi, hatimaye tunaweza kuwatazama,” anasema mmoja wa wanaakioloiia hao Daniel M Master.
“Kwa ugunduzi huu, tunakaribia kubaini siri za asili yao.”
Wanaakiolojia hao sasa wanafanya uchunguzi wa DNA pamoja na uchunguzi wa miale ya ukaa kubaini watu hao waliishi wakati gani.
Watafiti hutofautiana kuhusu asili ya Wafilisti, baadhi wakiamini walitoka Ugiriki, wengine visiwa vya Crete au Cyprus na wengine eneo la Anatolia nchini Uturuki.
Wafilisti huoneshwa katika Biblia kama maadui wakuu wa Waisraeli, na inadhaniwa walihamia Israel kutoka maeneo ya Magharibi karne ya 12 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu.
Anayefahamika zaidi ni Goliath, mpiganaji ‘jitu’ ambaye kwa mujibu wa Biblia, aliuawa na Daudi kabla yake kuwa Mfalme wa Waisraeli.
Katika Biblia, wanaoneshwa kama watu wakatili lakini mabaki yaliyopatikana yanaonekana kuashiria kwamba walikuwa na ustaarabu fulani.
CHANZO BBC
No comments:
Post a Comment