Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua rasmi semina ya wadau wa barabara mjini Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa semina ya wadau wa barabara iliyoanza mjini Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara hiyo sekta ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga kabla ya ufunguzi rasmi wa semina ya wadau wa masuala ya barabara mjini Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Daudi Felix Ntibenda kushoto akijadiliana jambo na mkuu wa mkoa wa Singida Mathew Mtigumwe kulia walipokutana katika semina ya wadau wa masuala ya barabara.
Wadau wa masuala ya barabara wakifuatilia kwa makini mijadala katika semina ya mikataba ya muda mrefu ya kupima huduma itolewayo na barabara na matokeo yake inayoendelea mjini Arusha.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa wa pili kushoto akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Arusha (AICC), wa pili kulia ni katibu mkuu wizara hiyo sekta ya Ujenzi Eng. Joseph Nyamhanga na wa kwanza kushoto ni mkuu wa mkoa wa Arusha Daudi Felix Ntibenda.
Imetolewa na kitengo cha habari na mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amewataka wahandisi na makandarasi nchini kujielimisha vya kutosha kuhusu mfumo mpya wa ujenzi wa barabara wa mikataba inayopima huduma zinazopatikana kwenye barabara hizo.
Mfumo huo ambao unaotumiwa na nchi zilizoendelea utawawezesha makandarasi nchini kujenga barabara kwa mkataba wa muda mrefu wa kupima huduma ya barabara na mkandarasi atalipwa kulingana na matokeo.
Akifungua semina ya wadau wa barabara kutoka nchi 19 na taasisi 30 duniani inaofanyika jijini Arusha Prof. Mbarawa amesema utaratibu huo mpya utawawezesha makandarasi kujenga barabara za kiwango cha juu zenye ubora na usalama na kupunguza utaratibu wa ukarabati wa kila wakati unaogharimu serikali fedha nyingi.
“Ukijenga barabara kwa viwango vya juu na ukiisimamia mwenyewe kwa muda mrefu itapunguza gharama za ukarabati wa kila mwaka zinazotolewa na serikali” amesema Prof. Mbarawa
Profesa Mbarawa amekiri uwepo wa changamoto kubwa kwenye ujenzi na ukarabati wa barabara za wilaya na kusisitiza kwamba barabara nyingi zinajengwa chini ya kiwango na hazina uwiano na thamani ya fedha zilizotumika.
“Serikali inajipanga kuanzisha wakala wa barabara za wilaya utakaohakikisha unafanya kazi kama ilivyo kwa wakala wa barabara kuu na za mikoa ili kuongeza ufanisi” amesema Prof. Mbarawa
Profesa Mbarawa amepongeza Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kwa kazi nzuri ya kusambaza fedha za ujenzi wa barabara katika halmashauri zote kwa wakati na kuwataka viongozi wa halmashauri hizo wazitumie fedha hizo kwa kazi zilizokusudiwa.
“Atakayecheza na fedha za mfuko wa barabara hatutakuwa na uvumilivu naye, tunataka fedha hizo zifanye kazi iliyokusudiwa ili adhma ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kwa kuwa na miundombinu bora ifanikiwe” amefafanua Prof. Mbarawa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, sekta ya ujenzi Eng. JOSEPH NYAMHANGA amesema semina hiyo ya siku tano inawaleta wataalam wa barabara nchini kujadili changamoto na mafanikio ya mfumo mpya ya ujenzi wa barabara na mfumo huo utakapoanza utapunguza gharama za ujenzi na kuwaongezea nguvu makandarasi wazawa.
Amesema Tanzania ina takribani ya km 87,481 za mtandao wa barabara ambapo km 35,000 ni barabara kuu na za mikoa, km 52, 581 ni barabara za wilaya ambapo zote zitanufaika na mfumo huo utakapoanza.
Naye meneja wa bodi ya mfuko wa barabara Joseph Haule amesema utaratibu huu mpya utakapoanza nchini utapunguza gharama za ujenzi wa barabara kwa asilimia 30 na utanufaisha wahandisi na makandarasi wengi nchini kutokana na sera nzuri ya kuwalinda makandarasi wazawa.
Takribani wataalam 200 wa masuala ya barabara kutoka nchi za Afrika, Ulaya na Amerika wanashiriki katika semina hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wa shirikisho la masuala ya barabara Bw. Kiran Kapila lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu katika masuala ya ujenzi wa barabara bora kwa gharama nafuu.
Imetolewa na kitengo cha habari na mawasiliano, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment